Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Wadau wa Afya unatarajia kuwa na kambi maalumu ya uchunguzi na tiba ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza kuanzia tarehe 17 hadi 21 Julai, 2018 katika uwanja wa Shycom, Manispaa ya Shinyanga.
Kambi hiyo maalumu ina lengo la kutoa huduma ya Upimaji wa Magonjwa, Kutoa Elimu ya Afya na ushauri kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na tabia ya kupima Afya zao kila wakati (Magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza) pamoja na kufanya uchunguzi wa Afya na kutoa huduma stahili za tiba / upasuaji kwa wananchi watakaothibitika kitaalam.
Wataalamu wa Afya wa ndani ya Mkoa na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali za Bugando, KCMC, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Mt. Thomas na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete watakuwepo kutoa huduma katika fani maeneo yafuatayo:- Upasuaji, Magonjwa ya ndani, Mfumo wa Mkojo(Urology)/Tezi Dume, Magonjwa ya akina mama, Magonjwa ya ngozi, Magonjwa ya Mfumo wa macho, koo, masikio na pua pamoja na Magonjwa ya watoto
Huduma zote za uchunguzi zitafanyika bila malipo. Wenye kadi za Bima za NHIF, CHF na nyinginezo watahudumiwa kwa kutumia kadi zao.
Wananchi zaidi ya 20,000 wanatarajiwa kufikiwa na kunufaika na huduma hii.
Wananchi wote mnaombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hili ili kupata huduma husika.
Imetolewa na:-
Zainab R. Telack,
Mkuu wa Mkoa,
Shinyanga
02 /07 /2018
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa