Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) amewataka waandishi wa habari Mkoani Shinyanga kuandika habari zenye Ajenda za Kitaifa ikiwamo ujenzi wa Miundombinu mbalimbali miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na kuhabarisha umma juu ya uwepo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wa 2024 sanjari na hatua ambazo zinaendelea kutekelezwa ikiwamo uboreshaji wa daftari la wapiga kura.
DC Mtatiro ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameyasema haya leo tarehe 29 Mei, 2024 katika Semina iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) na Umoja wa Klabu za Habari Tanzania (UTPC) katika ukumbi wa mikutano uliopo Karena Hotel hapa Manispaa ya Shinyanga huku akiwaahidi ushirikiano wakati wote na kwamba katika uongozi wake hapa hatokubali kuona mwanahabari akibughuziwa katika utekelezaji wa majukumu yake
"Pamoja na kuwapongeza sana Wanahabari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu ya Habari Tanzania (UTPC) kwa Semina hii nzuri ya Kijamii kuhusu Uhuru wa Kujieleza, lakini niwatake sasa kwenda kuandika habari zinazobeba Ajenda za Kitaifa ili umma uweze kuelewa," amesema DC Mtatiro.
Aidha, DC Mtatiro amesisitiza kwamba katika uhuru huo wa kujieleza unaotajwa basi uendane na mipaka sanjari na kuzingatia Sheria za nchi kwakuwa hakuna yeyote aliye juu ya sheria, na ili kukwepa kuingia kwenye mikono ya sheria, waandishi wanapaswa kuchakata habari zao kwa ufasaha na ziwe na uwiano wa pande zote mbili.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa SPC Bw. Greyson Kakuru amesema kuwa dhumuni la Semina hii ni kujadili kwa pamoja juu ya hali ya uhuru wa kujieleza kwa muktadha wa kusukuma na kuchochea maendeleo kwa sekta zote, ili kuona umuhimu wa uhuru wa kujieleza unavyoleta tija ya maendeleo hapa nchini.
Ndani ya Semina hii pia Mada mbalimbali zimejadiliwa ikiwamo ya Uhuru wa kujieleza, Utawala Bora kwa Maendeleo ya Mkoa wa Shinyanga, na Umuhimu wa upatikanaji wa Taarifa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa