Na. Shinyanga RS.
KATIBU Tawala Msaidizi (ELIMU) Mkoa wa Shinyanga Bi. Dafroza Ndalichako ambaye alimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo amefungua mafunzo ya mfumo mpya wa ununuzi NeST kwa wataalam 36 kutoka katika Halmashauri zote 6 zinazounda Mkoa wa Shinyanga huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote ndani ya Mkoa wa Shinyanga kusimamia na kutekeleza kwa weledi matumizi ya Mfumo huu mpya.
Bi. Ndalichako amewaeleza watalaam hao ambao walionesha utulivu na umakini wakati wote kuwa ujio wa mfumo huu mpya wa ununuzi unakwenda kuwa mwarobaini wa hujuma zilizokuwa zikijitokeza katika ununuzi na kuondoa kabisa urasimu ambao awali ulikuwa ukijitokeza huku akiwaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga kwenda kusimamia na kutekeleza kwa weledi mfumo huu katika maeneo yao ili tija ya mfumo huu iweze kuonekana.
"Nawaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri zetu zote 6 kwenda kusimamia na kutekeleza mfumo huu mpya ili uweze kuwa na tija kama ambavyo Serikali imekusudia," alisema Bi. Ndalichako.
Kando na maelekezo hayo, lakini pia Bi. Ndalichako aliishukuru sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya, pia aliwapongeza sana na kutambua mchango wa Mtendaji Mkuu (PPRA) Ndg. Joackim Maswi na Mamlaka yenyewe kwa kufadhiri na kufanikisha mafunzo haya ambayo yameanza leo hii tarehe 28 Agosti, 2023 katika ukumbi wa mikutano hapa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na yatafikia tamati tarehe 1 Sept, 2023.
PPRA walitoa mafunzo kama haya kwa maafisa kutoka Sekretarieti za Mikoa ya Tanzania Bara Jijini Dodoma kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuutumia mfumo ili na wao waweze kuwafundisha waliopo katika ngazi za Halmashauri ili nao wakawafundishe walipo katika maeneo yao ya kazi.
Picha ikionesha baadhi ya wakufunzi na wataalam wakiwa katika mafunzo ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa