Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya,maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto, Wizara ya fedha na mipango na wadau wa maendeleo imetoa jumla ya sh. Bil 2.6 kwa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kujenga na kukarabati vituo vya Afya 6 ili vituo hivyo viweze kutoa huduma za dharura za uzazi ikiwemo upasuaji.
Akizungumza katika ziara ya ufuatiliaji wa ukarabati wa vituo hivyo,Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya huduma za Ustawi wa jamii kutoka OR-TAMISEMI bw. Rasheed Maftaha ambaye anaongoza timu hiyo ya ufuatiliaji, amesema kuwa Serikali imeweka mkakati madhubuti wa kuimarisha vituo vya Afya 513 nchi nzima ili viweze kutoa huduma za dharura.
Maftaha amesema Serikali imeshapeleka fedha katika vituo 44 nchi nzima ambavyo vipo katika hatua ya ukamilishaji.
Aidha, vituo vingine 139 nchini vimeshapelekewa fedha kwa ajili ya kuanza ukarabati mara moja.
Mkoa wa Shinyanga umepata sh. 2.6 bil katika vituo vya Afya 6 ambavyo ni Songwa katika Wilaya ya Kishapu kilichopata sh. Mil 400.
Katika Wilaya ya Shinyanga vituo viwili vimepokea jumla ya sh. Mil 900 ambavyo ni Samuye sh. Mil 500 na Tinde sh. Mil 400, katika Wilaya ya Kahama kituo cha Chela kimepokea sh. Mil 400, Iyenze sh. Mil 500 pamoja na Ukune sh. Mil 400.
Katika awamu ya kwanza iliyotolewa mwezi Agosti mwaka jana 2017, kituo cha Afya Iyenze kilichopo Halmashauri ya Mji Kahama kipo katika hatua ya ukamilishaji, ambapo vituo vingine vya Songwa, Samuye, Tinde, Chela na Ukune vimeshaanza maandalizi ikiwemo kutenga maeneo ya ujenzi pamoja na uundaji wa kamati za kusimamia ujenzi huo kutoka kwenye uwakilishi wa wananchi.
Maftaha amesema mkakati huo wa sh. 1.3 trilioni unafadhiliwa na Benki ya dunia, Serikali ya Canada pamoja na Serikali ya Denmark ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa MMAM ambao kwa miaka 10 umekuwa haujatekelezwa kikamilifu.
Timu hiyo ya ufuatiliaji ipo Mkoani Shinyanga kwa siku 3 na imetembelea Wilaya zote tatu za Shinyanga, Kishapu na Kahama, kuona utekelezaji wa ukarabati wa vituo hivyo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa