Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola amesema takribani shilingi Bilioni 9 zitatumika kuijengea uwezo Taasisi, Watumishi na sehemu zingine katika kuboresha na kutoa huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wananchi Mkoani Shinyanga.
Ameyasema haya leo tarehe 4 Novemba, 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa miaka 4 wa kuijengea Taasisi uwezo baina yake na Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Gopa Infra ya Ujerumani ikishirikiana na Kampuni ya Superlit Consulting Ltd ya Tanzania, hafla ambayo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo makao makuu ya SHUWASA Manispaa ya Shinyanga.
“Kupitia Mkataba huu ambao tumesaini leo na Kampuni ya Gopa Infra naamini unakwenda kutimiza jukumu kubwa la kuijengea uwezo Taasisi yetu, watumishi na sehemu zingine ili kutekeleza uboreshaji na utoaji wa huduma za Majisafi na usafi wa Mazingira katika mkoa wetu wa Shinyanga” amesema Mha. Katopola.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Kampuni ya Gopa Infra Stefan Doerner, amefurahi kupata fursa ya kufanya kazi nchini huku akiahidi kuisaidia kuijengea uwezo SHUWASA ili kuhakikisha wanatoa huduma bora za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wananchi.
Mkataba huu ambao ni wa miaka 4 ni sehemu mojawapo ya mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye thamani ya Euro Milioni 76 ili kuwafikia wananchi wengi wapate huduma ya maji.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa