Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wajumbe wa Bodi mpya ya ushauri ya Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kutumia taaluma na uzoefu wao kusaidia uongozi wa Hospitali kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Akizindua Bodi hiyo mpya itakayodumu hadi tarehe 31/04/2019, Mhe. Telack amewaambia wajumbe hao kuwa wameaminiwa na kuteuliwa kuwakilisha wananchi katika kufanya maamuzi ya Hospitali ya Mkoa, hivyo hategemei watafanya kwa maslahi yao binafsi kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
"Bodi ya ushauri ya hospitali ya rufaa ya Mkoa ni chombo muhimu sana katika uendeshaji wa huduma za afya za hospitali za mikoa. Hiki ndicho chombo pekee kinachowaunganisha wananchi na Serikali yao katika ngazi ya hospitali ya rufaa ya Mkoa. Ni chombo ambacho kina wawakilisha wananchi katika kufanya maamuzi juu ya utoaji wa huduma katika hospitali ya rufaa ya Mkoa. Bodi inaweza kufananishwa na kioo ambacho menejimenti ya hospitali inakitumia kupata mrejesho wa namna wanavyotoa huduma kwa wananchi". amesema Mhe. Telack.
Mhe. Telack amesema, kazi kubwa ya Bodi ni kuishauri menejimenti ya hospitali na mamlaka zingine kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa kufuata Miongozo, Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi.
Ametoa angalizo kuwa, Serikali inahitaji bodi inayofanya kazi kwa ubunifu na kwa kujitolea. Sio bodi inayofanya kazi kwa kutegemea uwepo wa posho. "Kuna baadhi ya wajumbe wa bodi wa awamu zilizopita walikuwa wanagoma kuja kwenye vikao mpaka fedha za kuwalipa posho zitakapopatikana. Wajumbe wa namna hiyo kama wapo kwenye bodi hii basi ni vema wabadilishe mitazamo yao".
Aidha, Telack ameitaka bodi kuisaidia hospitali ili iweze kupata fedha zitakazosaidia kuendesha hospitali na kuibua fursa mbalimbali zitakazoboresha upatikanaji wa huduma bora na kuwa Serikali haitasita kuivunja bodi hiyo iwapo itashindwa kufanya kazi.
"Kwa kweli, Sisi upande wa Serikali hatutasita kuivunja bodi hii kama itashindwa kufanya kazi zake au itakuwa mzigo kwa hospitali kinyume na matarajio yetu".
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa Bw. Alfred Shayo amesema kuwa anaamini bodi hiyo itasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa watumishi, madeni ya wazabuni na watumishi pamoja na uchakavu wa miundombinu.
Bw. Shayo amesema pia kuwa, Serikali ipo tayari kushirikiana na bodi na kupokea ushauri utakaotolewa kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi.
Akitoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa kuzindua bodi hiyo, Mwenyekiti wa bodi Dkt. Ernest Haraka amesema bodi itajitahidi kutafuta suluhisho kwa changamoto zilizopo ikiwemo suala la watumishi na kutafuta mapato ili waweze kuwasaidia wananchi kwa njia yoyote ile kupitia wadau mbalimbali.
Dkt. Haraka ameahidi pia kuwa watazingatia yote waliyoelekezwa kwa kuyafanyia kazi jinsi ilivyokusudiwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa