Na. Paul Kasembo, SHY RS
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka wasimamizi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalotoa Elimu ya Usalama Barabarani kwa Jamii (AMEND) - Mkuza wa Bomba la Mafuta ghafi Afrika Mashariki (EACOP) kuhakikisha kuwa wanashirikisha wananchi wanapotekeleza mradi huu hapa mkoani Shinyanga ili kulinda usalama wao na mali zao katika maeneo ambapo mradi huu unatekelezwa.
Ameyasema haya leo tarehe 15 Novemba, 2024 kwenye kikao cha wadau wa Mkoa wa Shinyanga kikao ambacho kimelenga kuwashirikisha na kupokea mapendekezo kuhusu namna ya kuboresha usalama katika jamii ili kufanya Mkoa ubaki salama kwa muda wote ambao mradi wa EACOP utakuwa unatekelezwa.
“Niwaombe ninyi wasimamizi wa mradi wa EACOP na Shirika la AMEND kuhakikisha kuwa wakati mkitekeleza mradi huu wa bomba la mafuta katika Mkoa wetu wa Shinyanga, mnawashirikisha wananchi ili kulinda usalama wa afya zao na mali zao lakini pamoja na yote kuepukana na migogoro au ajali ambazo zitajitokeza katika utekelezaji wa mradi wenu”, amesema RC Macha.
Aidha RC Macha amewapongeza wasimamizi wa mradi wa EACOP na Shirika la AMEND kwa namna ambavyo wanashirikisha wananchi kuanzia katika hatua ya awali kabisa kupitia vikao na mikutano jambo ambalo limepekea kwa sasa wananchi kufahamu kila kitu kuhusu mradi huu tofauti na wakandarasi wengine ambao wamekuwa hawashirikishi wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi kutoka Shirika la AMEND Bi. Dilys Mneney amesema wameanza kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi na waendesha pikipiki katika maeneo ya mradi ili kuwasaidia EACOP hatua ya kuchukua endapo ajali ikitokea huku tathmini imekuwa ikifanyika pia ili kufahamu miundombinu ambayo inatumiwa na magari ya EACOP.
Akielezea hali ya usalama barabarani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga SACP Janeth Magomi amesema kwa sasa hali ya usalama ni nzuri ukilinganisha na miaka iliyopita kwani wanafanya kila wanaloweza na kutumia vifaa vya kisasa kubaini wanaovunja sheria za barabarani ili kuzuia ongezeko la ajali katika maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na ajali mara kwa mara.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa