Na Paul Kasembo, SHY RS.
WAZIRI wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (MB) amempongeza Mkurugenzi wa Gaki Investment Co. LTD ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba Tanzania ndg. Gasper Kileo kwa kuwa mwekezaji wa kuigwa ambaye ameleta mapinduzi makubwa katika zao la pamba huku akimtolea mfano mzuri wa utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ambaye ameajiri Maafisa Ugani Kilimo 15 wanaohudumia Kata 3 ya Kishapu, Meatu iliyopo Simiyu na Mbutu mkoani Tabora.
Mhe. Bashe ameyasema haya leo tarehe 12 Septemba, 2024 katika ziara yake ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Shinyanga ambapo pia amefika katika kiwanda kinachozalisha zao la pamba akiwa ameambatana na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamiringi Macha ambapo pia amesisitiza kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha uzalishaji wa zao la pamba unaongezeka zaidi.
“GAKI Investment ni moja kati ya wadau wakubwa wa zao la pamba ambaye anashiriki kwa kiasi kikubwa katika ununuzi wa zao na kuleta mapinduzi makubwa ya viwanda vya pamba nchini, lakini pia ametekeleza maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha wawekezaji wa bidhaa za kilimo wanaajiri Maafisa Ugani Kilimo ili waweze kuongeza tija katika Sekta ya kioimo kwani wao wamesomea na hivyo watasaidia kupitia taaluma zao” amesema Mhe. Bashe.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamiringi Macha amesema atakutana na Maafisa Ugani Kilimo wote pamoja na wadau wengine wa pamba ili kuhakikisha wanaendelea kutekekeleza maelekezo ya Serikali na kuhakikisha uzalishaji wa zao la pamba unaongezeka hatua kwa hatua.
“Katika hili, nami nitahakikisha ninakutana na Maafisa Ugani Kilimo ambao wamejiandaa vizuri wakiwa na vifaa vya kutosha tayari kwa kazi pamoja na wadau wengine wa pamba ili kuhakikisha tunatekeleza maagizo ya Serikali na kuhakikisha tunazalisha zao la pamba kwa wingi hatua kwa hatua” amesema RC Macha.
Naye Mkurugenzi wa Gaki Investment ndugu Gasper Kileo amesema wanafuata maelekezo ya Serikali kwa kutonunua pamba maeneo mengine na badala yake wananunua pamba katika maeneo waliyoelekezwa na wamefanikiwa kupata pamba ambayo imekidhi mahitaji ya msimu mzima.
“Tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kufuata maelekezo ya serikali ya kununua pamba maeneo ambayo tumeelekezwa na tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupata pamba ambayo inatusaidia kukidhi mahitaji yetu ya uzalishaji kwa msimu huu mzima” amesema Gasper.
Ikumbukwe kuwa Shinyanga ni moja kati ya Mikoa ambayo inazalisha zao la pamba hivyo kwa kufuata maelekezo ya serikali kuhusu zao hili uzalishaji wa pamba utaongezeka kwa kiasi kikubwa na utakuwa wenye tija zaidi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa