Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, imefanya ziara Mkoani Shinyanga na kukagua miradi mbalimbali leo tarehe 15 Machi, 2018.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jason Rweikiza imetembelea na kukagua ujenzi wa barabara ya lami katika Manispaa ya Shinyanga chini ya programu ya uimarishaji miji (ULGS) kwa ufadhili ya Benki ya Dunia ambayo inajengwa kwa gharama ya sh. bilioni 15.43 pamoja na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) katika kijiji cha Lunguya, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Kamati ikiwa kijijini hapo, Mwenyekiti Mhe. Rweikiza amegawa hati 5 za umiliki wa ardhi ikiwa ni sehemu ya hati 250 zilizoandaliwa na MKURABITA baada ya kupima mashamba 1,111.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika ambaye ni mjumbe wa Kamati hiyo, amesema lengo la MKURABITA ni kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi yao na kuitumia kupata kipato hivyo wanapimiwa mashamba yao na kupewa hati miliki waweze kukopesheka kwenye mabenki ili kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Kamati hiyo imepongeza hali ya Ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Shinyanga hususani kutokuwepo kwa mauaji ya Vikongwe na Albino.
Sambamba na hilo, Kamati pia imepongeza jitihada zinazofanywa na Mkoa na kuhakikisha uhakika wa chakula kwa kuwaelekeza wananchi na watumishi kulima angalau ekari 3 za mazao ya chakula na biashara.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa