Kamati ya lishe ya Mkoa wa Shinyanga imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa, Halmashauri zote zinatenga bajeti kupitia vyanzo vya mapato vya uhakika kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za lishe Mkoani hapa ili kukabiliana na tatizo la lishe.
Wakizungumza katika kikao cha kawaida cha kila robo mwaka, wajumbe wa Kamati hiyo inayoundwa na Wataalamu wa Sekretarieti ya Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na wadau wanaojishughulisha na huduma za lishe wamesema kuwa, moja ya sababu zinazofanya hali ya lishe kuwa mbaya Mkoani hapa ni pamoja na shughuli za lishe kutopewa kipaumbele katika mipango na bajeti.
Afisa lishe Mkoa Bw. Dennis Madeleke, akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu, amesema kuwa hakuna shughuli ya lishe iliyotekelezwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kwa kipindi hicho na kuongeza kuwa bado hali ya lishe siyo nzuri Kimkoa.
Kufuatia hali hiyo, kamati kwa pamoja imedhamiria kuhakikisha Halmashauri zote zinafuata muongozo wa Serikali wa kutenga kwenye bajeti sh. 1000 kwa mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa huduma za lishe kwa kila mtoto wa chini ya miaka 5.
Awali akifungua kikao cha kamati hiyo, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya katika Sekretarieti ya Mkoa Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa changamoto bado ni kubwa hasa kwa akinamama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kuwa na upungufu wa damu ambapo amesema asilimia 59.4 ya akinamama wajawazito kwa mwaka wanakuwa na tatizo la upungufu wa damu wakati wa kujifungua hivyo kusababisha vifo. Aidha, watoto chini ya miaka mitano ni asilimia 7.
Pamoja na mkakati huo wa kutenga bajeti, kamati ya lishe pia imeazimia kuendelea kushirikiana na wadau wanaojishughulisha na huduma za lishe kwa kuhakikisha wadau hao wanatumia Wataalamu wa Serikali katika kutekeleza majukumu yao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa