Na Shinanga RS
KAMATI ya Maafa ambayo iliundwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kufuatia janga la kubomoka kwa kingo katika Bwawa la Majitope katika Mgodi wa Almasi Mwadui uliopo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, na kuleta athari kwa wananchi na kupoteza mali mbalimbali ikiwemo mashamba na baadhi ya nyumba, imeridhishwa na namna ambavyo ulipwaji wa fidia kwa wananchi ulivyofanyika.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hii ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude mara baada ya kufanya ziara katika Mgodi huo ili kupata taarifa juu ya hatua ya ulipwaji fidia wananchi hao ikiwa ni pamoja na waliokuwa wakidai nyumba zao, sanjali na kukagua ujenzi wa bwawa jipya la Majitope pamoja na kuona Maendeleo ya uzalishaji Almasi katika mgodi huo.
"Kwa ujumla tumeridhishwa na namna ambavyo zoezi la ulipaji wa fidia kwa waathirika wa Majitope katika mgodi huu wa Mwadui ambao ni takribani kaya 304 na kwamba huyu mmoja ambage hajapatikana juhudi ziendelee za kumtafuta ili kumpata na apate stahiki yake," alisema Mhe. Mkude.
Awali akiwasilisha taarifa ya ulipwaji fidia wananchi na maendeleo ya uzalishaji wa Almasi, Mhandisi Mkuu wa Mgodi wa Mwadui Shagembe Mipawa, akimwakilisha Meneja Mkuu wa Mgodi huo, amesema tatizo la kupasuka kingo za Bwawa la Majitope lilitokea Novemba mwaka jana na Wananchi 304 waliathirika na tope hilo.
Amesema mpaka sasa mgodi umefikia asilimia 99.6 kwamba ya ulipaji fidia ambapo kati ya wananchi 304 waliopaswa kukipwa, ni mwananchi 1 tu ndiye ambaye hajalipwa fidia yake na kwamba hajulikani alipo mpaka sasa, huku mgodi ukiendelea kumtafuta sanjali na kuendelea na taratibu zingine za ujenzi wa Makazi Mbadala ya nyumba 47 na kuhamisha Makaburi 14.
Akizungumzia suala uzalishaji wa Almasi, amesema wanaendelea vizuri na tangu waanze uzalishaji Julai mwaka huu hadi kufikia Mwezi Septemba wamezalisha Tani Milioni 1.4 sawa na asilimia 48, Carati Laki 106 sawa na asilimia 64 ya malengo yao.
Pia amewahakikishia wananchi kwamba Bwawa hilo Jipya la Majitope ni salama kabisa, huku wakiendelea pia kulifanyia ukaguzI wa mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Kamati ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude (katikati) akielezea jambo wakati kamati ilipotembelea eneo la mgodi
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa