Kamishna wa Uraia na Paspoti nchini, Gerald Kihinga, amefanya ziara rasmi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, Mhe. Mboni Mhita, ikiwa ni sehemu ya kujadili maboresho ya huduma za Uhamiaji katika mkoa huo.
Katika mazungumzo yao, Kamishna Kihinga alieleza dhamira ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Uhamiaji ya kuhakikisha huduma za uraia na paspoti zinaendelea kuimarika kwa wananchi, huku akielezea jitihada za kupeleka teknolojia mpya na kuongeza ufanisi katika utoaji wa paspoti na vitambulisho vya uraia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mhita alimpongeza Kamishna huyo kwa kufika mkoani humo na kueleza kuwa ushirikiano baina ya serikali za mikoa na taasisi za kitaifa ni muhimu katika kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati.
Aidha, aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Idara ya Uhamiaji ili kuhakikisha mkoa unakuwa salama na wenye kutoa huduma bora kwa wananchi na wageni wanaoingia nchini kupitia maeneo ya mipakani au kutoka mikoa jirani.
Ziara hiyo pia ililenga kufuatilia utekelezaji wa mikakati ya utoaji wa paspoti mpya za kielektroniki, pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma hizo ili ziweze kutatuliwa kwa haraka.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa