Na Johnson James, Shinyanga
Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Bakari Kasinyo, ametoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na uzalendo mkubwa ili kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 unafanyika kwa amani, haki na uwazi.
Akizungumza Oktoba 27, 2025 baada ya kutembelea kituo cha mafunzo cha Ukenyenye, Wilayani Kishapu, Kasinyo amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewaamini maafisa hao kusimamia mchakato nyeti wa kidemokrasia, hivyo hawapaswi kufanya makosa au kuruhusu upendeleo wa aina yoyote.

“Mafunzo mnayoyapata ni ya msingi sana. Mnatakiwa kuyatumia kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa ufanisi na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Nawasihi mfanye kazi hii kwa moyo wa kizalendo na kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu,” alisema Kasinyo.
Jumla ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi 1,726 wanapatiwa mafunzo ya siku mbili yaliyoanza Oktoba 26 hadi 27, 2025 katika Jimbo la Kishapu, ambapo jumla ya vituo 556 vya kupigia kura vimeandaliwa kwa ajili ya uchaguzi huo.

Kwa upande wao, baadhi ya wasimamizi wakiongozwa na Joel Lwasye, wamesema mafunzo hayo yamewaongezea maarifa na ujasiri wa kusimamia zoezi la upigaji kura kwa ufanisi, huku wakiahidi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na uwazi ili kupatikana kwa viongozi bora.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa