Na. Paul Kasembo, SHY RS.
Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga Bi. Mwamba Masanja amesema kuwa wameshughulikia kero ya ubovu wa barabara ya Isoso- Mwabusiga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu iliyokuwa inakarabatiwa na kampuni ya Advance Construction Ltd chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Kishapu.
Ameyasema haya leo tarehe 13 Novemba, 2024 wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya utendaji kazi wa Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha robo ya kwanza (1) Julai – Septemba kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wake wa kawaida wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.
“Kumekuwa na changamoto za wakandarasi kutekeleza miradi ya barabara chini ya kiwango kinyume na mikataba wanayoingia na Serikali, hivyo TAKUKURU tuliipata taarifa hii na tumefanikiwa kushughulikia kero ya ubovu wa barabara ya Isoso - Mwabusiga iliyopo Kishapu ambayo Kampuni ya Advance Construction Ltd ilikuwa ikikarabati”, amesema Bi Mwamba
Aidha ameongeza kuwa watuhumiwa hao ambao wamehusika na ukarabati wa barabara ya Isoso – Mwabusiga ambao ni Mhandisi Juma Mkela msmamizi mkuu wa kampuni ya Advance Construction, Mhandisi wa mafunzo TANROAD Shinyanga Charles Emmaneul pamoja na Mhandisi Wilfred Gutta Meneja wa TARURA Kishapu, tayari wamefikishwa mahakamani na kuamriwa kurejesha kiasi chote cha fedha Shilingi Milioni 29.
Aidha Bi Mwamba amewaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kupiga simu bure namba 113 ili kuripoti vitendo vinavyoashiria ubadhilifu wa fedha za miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Shinyanga.
TAKUKURU inaendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuhakikisha miradi yote inayoendelea katika Mkoa wetu inakamilika kwa ubora kama ilivyopangwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa