Na Paul Kasembo, Shy Rs.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamiringi Macha amewatakia wanafunzi wa darasa la saba Mkoa wa Shinyanga maandalizi mema ya mtihani wao wa kumaliza elimu ya shule ya msingi ambao utaanza siku ya kesho tarehe 11-12.09.2024.
Ameyasema hayo leo tarehe 10 Septemba, 2024 huku akibainisha watahiniwa takribani 45,693 wanaotarajiwa kufanya mtihani wakiwemo wavulana 19,528 na wasichana 26,165 katika shule za msingi za serikali 593 na shule za msingi 61 za binafsi.
“Ninawatakia wanafunzi wote maandalizi mema ya mtihani wa kumaliza elimu ya shule ya msingi utakaoanza kesho tarehe 11 Septemba, 2024 nikiamini mtaenda kufanya vizuri na kukumbuka yale yote mliyojifunza kwa miaka saba shuleni na niwapongeze kwa uvumilivu mkubwa ambao mmeuonesha pamoja na changamoto zozote mlizokumbana nazo” amesema Macha.
Pia amewataka walimu, wazazi na wanafunzi kutokujihusisha na udanganyifu wa aina yoyote wakati wa mtihani na badala yake wanafunzi watumie yale ambayo walijifunza wakiwa darasani ili kujibu mtihani na kupima uwezo wao.
“Niwasihi walimu, wazazi na wanafunzi kuepuka kabisa kujihusisha na udanganyifu wa aina yoyote wakati wa mtihani kwani ni kosa kubwa kisheria na badala yake muwasaidie wanafunzi wakumbuke yote waliyojifunza darasani na wafanye mitihani kwa kutumia akili zao wenyewe ili kupima uwezo wao” ameongeza Macha.
Kwa ujumla maandalizi ya mtihani huo yamekamilika na wanafunzi 45,693 ndani ya Mkoa wanatarajia kufanya mtihani wao wa kuhitimu elimu ya shule ya msingi ambapo wavulana ni 19,528 na wasichana 26,165, aidha walimu watakaosimamia mtihani huo ni 3,339.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa