Repost @shinyanga_press_club
KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC),imefanya Mkutano Mkuu wa Wanachama wake , huku Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, ikiahidi kuendelea kushirikiana na Vyombo vya Habari pamoja na kutoa mafunzo ya namna ya uandishi wa habari za Kimahakamana kwa kuzingatia Sheria na Miongozo yake.
Mkutano huo umefanyika leo Aprili 5, 2025 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, huku Mgeni Rasmi akiwa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Ntuli Mwakahesya akimwakilisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo Mhe. Frank Mahimbali.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga ndg. Greyson Kakuru akisoma taarifa ya Klabu hiyo kwa Mgeni Rasmi, alisema mkutano huo ni takwa la kikatiba kwa ajili ya kujadiliana maendeleo ya ustawi wa klabu.
“Katika mkutano wetu huu mkuu leo tutajadili taarifa za maendeleo ya klabu yetu na kufanya maamuzi ya kimuundo kwa utawala kwa kupitisha bodi ya klabu ili tuendane na mabadiliko ili kuwa na klabu ya ustahimilivu wa kusonga mbele zaidi,”alisema Kakuru.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi Mhe. Ntuli Mwakahesya ameipongeza SPC kwa mkutano wao pamoja na kuwa miongoni mwa Klabu bora hapa nchini huku akiahidi kuwa Mahakama hiyo itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari na kwamba itaandaa mafunzo kwa waandishi wa habari ya namna bora ya kuandika habari za Kimahakama huku wakiwasihi wanahabari wawe wanafika Mahakamani na kuandika habari na kuhabarisha umma.
Katika kuelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu Mhe. Ntuli amewsihi wanahabari kuandika taarifa zenye kuzingatia maadili na miiko ya taaluma zao pamoja na kuhakiki vyanzo vya taarifa viwe vyenye usahihi na kuaminika.
SPC imetoa shukrani za dhati kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,TASAF, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, jambo Group, SHIDEFA, BENKI ya CRDB, Life Water, RUWASA, SHUWASA, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Jeshi la Zimamoto na uokoaji, huku wito ukitolewa na wakiwakaribisha wadau wengine kushirikiana na SPC.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa