Shinyanga, Mei 26, 2025 – Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro (Wakili), kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, amewataka wastaafu kuzingatia utulivu na ustawi wa maisha baada ya kustaafu, akisisitiza kuwa kipindi hicho ni muda wa kupumzika baada ya utumishi wa muda mrefu kwa Umma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Umoja wa Wastaafu Tanzania (Retirees’ Association of Tanzania - REAT) Mkoa wa Shinyanga, iliyofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa, Mhe. Mtatiro amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushughulikia changamoto za wastaafu na kuwashirikisha katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Mhe. Mtatiro amewahimiza wastaafu kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili kuanzisha miradi endelevu, huku akibainisha kuwa Serikali ipo tayari kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo ili kuwawezesha kuendeleza maisha yao kwa heshima na utu.
Aidha, ametoa rai kwa wazee kushiriki katika kulinda maadili ya jamii kwa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile ubakaji na ulawiti, na kuwahimiza kutoa malezi bora kwa watoto kwa kuzingatia tahadhari mbalimbali ndani ya familia. Pia amesisitiza umuhimu wa kuandika wosia, akieleza kuwa ni hatua muhimu ya maandalizi ya maisha baada ya wao kuondoka.
Vilevile, Mhe. Mtatiro amewaasa wazee kuwa mabalozi wa amani na kuhimiza ushiriki wa vijana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wake, Rais wa Umoja wa Wastaafu Tanzania (REAT), Alhaj Dauda Bilikesi, amesema lengo kuu la umoja huo ni kuimarisha mshikamano, kutambua mchango wa wastaafu kwa Taifa na kuendeleza utetezi wa haki na maslahi yao baada ya utumishi.
Akiwasilisha risala ya REAT, Mwalimu Mstaafu Magdalena Faustine alisema umoja huo unalenga kuwaunganisha wastaafu, kushirikiana na Serikali katika kutetea haki zao, na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi, sambamba na kutoa elimu kuhusu haki zao.
Mratibu Mkuu wa REAT, Mwalimu Ezekiah Oluoch, alieleza kuwa Umoja huo ulianzishwa mwaka 2021, na unawahusisha wastaafu kutoka sekta ya umma na binafsi wanaopokea mafao kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSSF, NSSF na Hazina.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa