Na. Paul Kasembo.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Seleman Jafo amesema kuwa ujio wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani umewawezeaha na kuwaongezea fursa zaidi wakulima nchini wakiwemo wa Mkoa wa Shinyanga.
Mhe. Dkt. Jafo ameyasema hayo leo Machi 13, 2025 wakati akitoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyotembelea na kukagua utekelezaji wa maelekezo ya Serikali juu ya matumizi sahihi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ambapo Kamati imeshuhudia hayo katika Ghala la Mboje lililopo Manispaa ya Shinyanga na kusisitiza kuwa mfumo unaongeza ushindani zaidi miongoni mwa wanunuzi.
"Mhe. Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati, nipende kusema kuwa ujio na matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani umekuja na ongezeko la fursa nyingi zaidi kwa wakulima wetu kwa kuwa hivi sasa wanunuzi ambao ndiyo wafanyabiashara wananunua kwa ushindani sana kulingana na msimamo wa bei ya soko na wingi wao. Na hilo ndiyo lilikuwa lengo kuu la Serikali kuhakikisha mkulima anaanza kunufaika na kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo ya Choroko na Dengu hapa Shinyanga," alisema Dkt. Jafo.
Akitoa ufafanuzi, umuhimu na faida ya matumizi ya mfumo, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani ndg. Asangye Bangu alisema kuwa katika mikoa ya Kagera, Mwanza na Shinyanga mfumo haukuweza kutumika kutokana na kutokuwa tayari kwa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha alimueleza Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati kuwa, awali haikuwa kazi rahisi sana kufikia maridhiano kati ya Serikali ya Mkoa na Wafanyabiashara na kuanza kwa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala mkoani Shinyanga. Lakini baada ya majadiliano na utoaji wa elimu kwa kushirikiana na wataalam wa WRRB waliweza kufanikiwa na sasa Serikali imeanza kuona mapinduzi makubwa ya wakulima na wafanyabiashara ambapo pande zote zinanufaika.
Akihitimisha ukaguzi wa Ghala na kuona faida ya matumizi ya mfumo, Mhe. Deodatus Mwanyika (MB) ambaye ni Mwenyekiti kwa niaba ya Kamati amekiri kuridhishwa na utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ya ghala hususani mkoani Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa