Na. Shinyanga RS.
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi amefugua rasmi shule ya msingi Shilabela iliyopo Kata ya Ulewe Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoani shinyanga huku akiwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwakuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekwisha watengenezea miundombinu yote ya elimu, kuwaletea waalimu na kuwaletea vifaa vya kusomea pamoja na samani zake.
Hayo yamesemwa leo tarehe 19 Agosti, 2023 na Mhe. Ndejembi ambaye alimuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Angellah J. Kairuki wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya Sekta ya Afya ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu iliyopo Kata ya Nyamilangano iliyojengwa kwa fedha za Serikali Kuu na baadae alikwenda kufungua shule ya msingi Shilabela iliyojengwa kwa thamani ya Tzs. 561,100,000/= fedha za Boost 2022/2023.
"Hongereni sana kwa kufanikisha ujenzi wa shule hizi mpya ambapo leo nimefungua rasmi shule ya msingi Shilabela hapa Kata ya Ulewe Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu hapa Mkoani Shinyanga, tunampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza yote haya, kwa kuwajali wana Ulewe na hata kuwajengea shule mpya, kwa hiyo sasa jambo moja nawataka wanafunzi wetu msome kwa bidii maana Serikali ya awamu ya sita imetekeleza kila kitu ikiwamo miundombinu ypte ya elimu, kuwaletea walimu na vifaa vya kujifunzia nanyi wajibu wenu sasa ni kusoma kwa bidii tu," alisema Mhe. Ndejembi.
Awali akizungumza baada ya kukagua shule mpya ya Bugomba 'A' Mhe. Ndejembi alisema kuwa ni vema kamati za ujenzi, kamati za shule na wataalamu wote kuwa na utamaduni wa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote na siyo kuwaachia mafundi peke yao kama ambavyo ilionekana kasoro katika umaliziaji wa madirisha jambo ambalo aliagiza ziondolewe na kuwekwa nyingine mpya ndani ya siku 14.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita @mboni.mimi alimshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Ushetu na kuwaletea maendeleo ya kweli katika sekta zote ikiwemo na elimu.
Mhe. Mboni alimshukuru pia Naibu Waziri Ndejembi huku akimuahidi kuwa yale yote aliyoelekeza, aliyoagiza ameyachukua na atayafanyia kazi haraka, weledi na kwa wakati zaidi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe. Emmanuel Cherehani alimshukuru sana Mhe. Ndejembi na kumuoba amfikishie salamu za wana Ushetu kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake wa dhati kwa wana Ushetu hata kuwajengea Hospitali ya Ushetu, Shule mpya, madarasa na miundombinu, samani zake sambamba na kuwasogezea huduma karibu ya maji, barabara na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Mkoa wa Shinyanga unasimamia na kuratibu Elimu kuanzia ngazi ya Awali hadi Vyuo Vikuu. Mkoa una madarasa ya awali 672, shule ya msingi 672, shule ya sekondari 172, Chuocha Ualimu 1, Vyuo Vikuu 2, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii 2 na Chuo cha Veta 1 na Vyuo vingine 2 ambavyo vinaendelea kujengwa katika Halmashauri ya Kishapu na Msalala.
Picha ikionesha Shule ya Msingi Shilabela
Picha ikimuonesha Mhe. Ndejembi akiongea na baadhi ya watumishi nje ya jengo la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa