Na. Shinyanga RS.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (MB) amezitaka Kamati za Uendeshaji Afya ngazi ya Wilaya na Mkoa kwenda kuhudumia na kutatua kero zinazowakabili wananchi badala ya kubakia ofisini au kutumia muda mwingi kwenye Semina na Makongamano.
Mhe. Ummy ametoa maelekezo haya wakati akizungumza na wataalamu wa afya Mkoa wa Shinyanga katika ziara yake ya siku ya kwanza ambapo kikao hicho kilijumlisha wataalamu kutoka katika Halmashauri zote 6 za Mkoa wa Shinyanga.
"Nazitaka Kamati zote za CHMT na RHMT kutoka maofisini na kwenda kuhudumia na kutatua kero za wananchi na mpunguze kahisa Semina na Makongamano ya mara kwa mara jambo ambalo linachukua muda mwingi zaidi kuliko kutatua kero, nilisema nikiwa Simiyu na leo narudia hapa Shinyanga," alisema Mhe. Ummy.
Aidha Mhe. Ummy amewataka watunza dawa wote kuhakikisha wanaondoa kero zinazo wakabili wananchi katika upatikanaji wa dawa huku akisema kuwa sababu kubwa ni kwamba hawaombi dawa kwa wakati hivyo kupelekea malalamiko kwa wananchi na kuwataka wajitathimini kwa hilo huku akisema kuwa Wizara imetoa muongozo kuanzia sasa dawa za kutibu shinikizo la damu zipatikane ngazi ya zahanati na siyo lazima mtu aende hosp kubwa kwa Serikali inatoa dawa kwa 100%.
"Tangu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameingia madarakani Sekta ya Afya inapata %100 ya fedha za dawa na vifaa tiba, na huu ni mwaka wangu wa 7 sàsa nikiwa kama Waziri wa Afya lakini sijaona tukipata %100 ya dawa kama kwenye kipindi hiki cha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na katika hili nisisitize vipimo vyote vipatikane tena kwa wakati," alisisitiza Mhe. Ummy.
Katika hatua nyingine Mhe. Ummy amewataka wataalamu kutoa huduma kwa wakati ili kuondokana na kutumia muda mrefu kwa wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma, hivyo akaagiza kuanzia sasa wahudumu wote kuanza kutoa huduma kwa haraka kuepusha wagonjwa kukaa muda mrefu.
Lugha na kauli nzuri ni moja kati ya maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Ummy kwa wataalamu wa afya wakati wanawahudumia wagonjwa huku akiwataka kuzingatia maadili ya kitaaluma zaidi na atakayebainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za Mabaraza ya Kitabibu hivyo akawataka kuzingatia maadili ya kitaalamu.
Katika hatua nyingine Mhe. Ummy ameipongeza Shinyanga kwa kuwakinga wasichana na Saratani ya Mlango wa Kizazi ambapo Mkoa unaanza kwa wasichana wenye umri wa miaka 13 huku akisema kuwa chanjo hii ni salama kabisa na haina madhara yoyote kwa afya zao sambamba na kuimarisha utoaji huduma ya Mama na Mtoto ambapo pia aliipongeza Shinyanga kwa kufanya vizuri pia.
Kando na hayo Mhe. Ummy aliipongeza Manispaa ya Shinyanga kwa ujenzi wa Jengo la Idara ya Dharula na kwa kuweza kutenga fedha nyingi kwa ajili ya watumishi wa mkataba kwa sekta ya afya ambapo zaidi ya Milioni 70 imetengwa huku akitaka Huduma za Uangalizi kwa Watoto Wachanga kuhakikisha zinatolewa kwa kila Halmashauri.
Aidha pongezi nyingi zimetolewa kwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa huduma nzuri, bora na yenye viwango kwa wananchi wa Mkoa huku akiwataka lkuongeza juhudi zaidi kwa kuzingatia weledi, taaluma, maadili, kanuni na sheria za kitabibu katika utendaji kazi wao.
Picha ikimuonesha Mhe. Ummy Mwalimu akielezea jambo wakati alipozungumza na wataalamu wa CHMT na RHMT Mkoa wa Shinyanga
Mhe. Johari Samizi ambaye ni Mkuu wa Wilaya alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme katika kikao cha Wazriri wa Afya
Picha ikionesha sehemu ya wataalamu wa afya Mkoa wa Shinyanga walipokuwa kwenye kikao na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa