Na. Paul Kasembo, SHY RS.
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Mkandarasi anayefanya Ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga aitwae China Hennan International Corperation Group Co. Ltd (CHICO) kuagiza taa na kuzifunga haraka ili uwanja utakapoanza kutumika uweze kufanya kazi masaa 24 na ukizingatia CHICO hadai pesa yoyote katika Kandarasi hii inayotajwa kuwa bora na yenye tija zaidi kwa Mkoa wa Shinyanga, Simiyu, Geita na maeneo jirani kwa ujumla.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo leo februari 16, 2025 baada ya kukagua ujenzi wa jengo la abiria lililopo uwanja wa ndege wa Shinyanga na ambalo ujenzi wake umetajwa kufikia asilimia 50 kukamilika huku akimsisitiza CHICO kuongeza kasi ya ujenzi na kufanya afanye kazi usiku na mchana lengo likiwa ni kukamilisha mradi huu kabla ya mwezi wa 8 uliotajwa katika mkataba.
"Wito wangu kwako Mkandarasi CHICO, agiza taa na uzifunge hapa uwanjani haraka kwani uwanja huu utakuwa ukifanya kazi masaa 24 na ukizingatia una viwango vyote vya Kimataifa na ndiyo maana Serikali iliongeza fedha za kuongeza urefu wa njia ya kuruka na kutua kutoka KM 2 hadi 2.2," amesema Mhe. Majaliwa.
Akimkaribisha kukagua jengo hilo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Mwambungu alimueleza Mhe. Majaliwa kuwa, katika kuhakikisha ukarabati mkubwa unafanyika, zaidi ya Milioni 700 zililipwa kwa wananchi wa maeneo hayo ili kupisha utekelezwaji wa mradi huo mkubwa na wa kimkakati zaidi kwa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani.
Mha. Joel alisisitiza kuwa, uwepo wa mradi huu mkubwa umewezesha wananchi takribani 160 kupata ajira za muda huku 130 kati ya hao ni wazawa wa Shinyanga.
"Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, katika kuhakikisa mradi huu mkubwa na wa kimkakati unatekelezeka bila malalamiko, Serikali iliwalipa Tzs. Milioni zaidi ya 700 wananchi wa maeneo haya ya Ibadakuli hapa Manispaa ya Shinyanga ili kupisha mradi huu kutekelezwa, na pia zaidi ya wananchi 160 walipata ajira ya muda huku 130 kati ya hao ni wazawa wa Mkoa huu wa Shinyanga," amesema Mha. Joel.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa