Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amemtaka mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kusambaza umeme wa REA Mkoa wa Shinyanga kujitahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia ubora kwani miundombinu haina changamoto zozote.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 5 Novemba, 2024 wakati wa utambulisho wa mkandarasi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kusambaza umeme Vijijini katika Vitongoji 90 ambao utanufaisha kaya 2970 Mkoani Shinyanga kupitia kampuni ya wazawa ya Derm Group Ltd ya Jijini Dar Es Salaam.
“Nikupongeze mkandarasi kwa kushinda zabuni hii ya kusambaza umeme kwenye Vitongoji 90 vilivyopo katika mkoa wetu wa Shinyanga lakini nikuagize kwenda kutekeleza mradi huu kwa wakati uliopangwa na kuzingatia ubora wa hali ya juu kwa sababu miundombinu ni salama na haina changamoto zozote ambazo zinaweza kukukwamisha kufanya kazi hii kwa weledi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi Mha. Robert Dulle ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa Shilingi Bilioni 11 zitumike kusambaza umeme kwenye Vitongoji 90 Mkoa wa Shinyanga huku akieleza kuwa tayari maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza.
Akizungumza baada ya utambulisho, Meneja wa mradi wa kampuni ya Derm Group Ltd Mha. Justinus Mutalemwa amesema mpaka sasa mradi huu unaendelea kutekelezwa na utakamilika baada ya muda mfupi kabla ya miezi 24 iliyopangwa kukamilika kwani hakuna changamoto zozote zilizojitokeza.
Mradi huu wa kusambaza umeme kwenye Vitongoji 90 unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 ambapo utekelezaji ulianza Septemba 20224 na utakamilika tarehe 19 Agosti, 2026 katika majimbo 6 kutoka Wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu na utanufaisha kaya 2,970 kwa Mkoa mzima.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa