#shinyanga_rs
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Lazaro Twange, amefanya ziara rasmi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kujitambulisha kwa Mhe. Anamringi Macha pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya TANESCO na uongozi wa Mkoa.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga. Mha. Twange alieleza kuwa TANESCO inaendelea kuboresha huduma zake na kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi bora ya umeme, hasa kwa kutumia vifaa vinavyotumia nishati kidogo.
Akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mha. Twange alikabidhi rasmi jiko la kisasa linalotumia umeme kwa kiwango kidogo kwa Mhe. Anamringi Macha, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya shirika hilo katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, rafiki kwa mazingira na nafuu kwa matumizi ya kawaida ya nyumbani.
"Jiko hili ni suluhisho linalolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa mazingira na afya ya wananchi," alisema Mhandisi Twange.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Anamringi Macha, alimshukuru Mkurugenzi huyo kwa ujio wake na zawadi ya jiko hilo. Aliahidi kuendelea kushirikiana na TANESCO katika kampeni za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kufikia malengo ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa