Mkuu wa Mkoa avunja Serikali ya kijiji Maganzo
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameivunja Serikali ya kijiji cha Maganzo pamoja na Kamati shule ya Msingi Jitegemee na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kukagua mapato yote na matumizi ya kijiji hicho ikiwemo fedha zilizochangwa na kutumika kujenga choo na madarasa yaliyochimbwa almasi na kufanya tathimini ya uharibifu uliojitokeza.
Mhe. Telack amefikia uamuzi huo jana wakati wa ziara yake Wilayani Kishapu, kufuatia kitendo cha wajumbe wa Kamati ya shule ya msingi Jitegemee pamoja na Serikali ya kijiji kuchimba madini kwenye vyumba vya madarasa yanayojengwa kwa lengo la kutafuta Almasi.
“Kwa utaratibu mimi ndiye mwenye mamlaka ya kuvunja Serikali ya kijiji na kuanzia leo nimesema Serikali ya kijiji hicho naivunja, tutafanya taratibu za kuchagua Serikali nyingine” amesema Mhe. Telack.
Amesema wote waliohusika wawajibike kulipa hasara hiyo kwani siyo hasara ya Serikali. Wajaze vifusi na waweke mawe ndani ya madarasa hayo kadri ya maelekezo ya wahandisi wakati taratibu za mahakama zikiendelea.
Viongozi wa kijiji cha Maganzo wanatuhumiwa kuhusika kuchimba ndani ya vyumba vya madarasa yanayojengwa kwa nguvu za wananchi katika shule ya msingi Jitegemee kwa madai ya kutafuta madini ya Almasi pamoja na tuhuma nyinginezo ikiwemo kumkashifu Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba kuwa hafai kuongoza Wilaya hiyo.
Wakati huo huo, Mhe. Telack amewataka matajiri wanaowatuma vijana maarufu kwa jina la “wabeshi” wanaoingia kwenye migodi kwenda kuiba mchanga wa almasi uliokwisha chimbwa kuacha mara moja tabia hiyo kwani Serikali haitawavumilia na haitawaacha imejipanga kuwakamata wote.
“Mkawaambie, wakati wao umekwisha, hatutawavumilia na hatutawaacha nadhani mshaona kazi tunayofanya kwa sasa, tuna kikosi maalumu kwa ajili ya kudhibiti wabeshi. Tutawakamata kila mmoja na kuhakikisha Maganzo ni sehemu salama ya kuishi siyo hatarishi”. Amesema Telack.
Amesema watu wote wanaotumia fedha zao kuleta uvunjifu wa amani wajue biashara hiyo imeisha kwani watapambana na Serikali, watafute shughuli nyingine za kufanya na watafute mali halali siyo kwa mtindo huo.
Amemtaka Mkuu wa kituo cha polisi Wilaya ya Kishapu awakamate wahalifu wote Maganzo wakiwemo viongozi wanaoongoza kwa uvunjifu wa Amani.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa