Asasi ya kitaifa ya “Thubutu Africa Initiative” imetambulisha mradi wa kuwasaidia wasichana waliopevuka kupata kwa urahisi pedi za bei nafuu ili ziwasaidie kipindi cha hedhi.
Akizungumza wakati wakutambulisha mradi huo, ambao utaanza kwa majaribio Mkoani hapo kwa miezi mitatu, Mkurugenzi Mtendaji wa mradi Bw. Jonathan Kifunda amesema changamoto kubwa iliyopo katika jamii nyingi ni kuwa, wazazi hawazungumzi na watoto wa kike kuhusu hedhi matokeo yake watoto wengi wanaingia kwenye hedhi bila taarifa, hivyo wanakutana na madhara mengi ikiwemo kuchekwa na wenzao mashuleni hatimaye wanashindwa kujiamini hata kuogopa shule.
Bw. Kifunda amesema kutokana na utafiti uliofanywa na shirika la SNV kanda ya ziwa mwaka 2014, asilimia 82 ya watoto wa kike wanaingia kwenye hedhi bila kujitambua, wakati asilimia 70 ya utoro mashuleni unasababishwa na wanafunzi wa kike kushindwa kuhudhuria masomo siku za hedhi.
Amesema pia kuwa, wazazi asilimia 60 hawazungumzi na watoto wao kuhusu hedhi lakini wako tayari kuwaunga mkono watoto wao iwapo pedi za bei nafuu zitapatikana ili waweze kuwanunulia.
“Kama suala la hedhi ni la kuficha, sisi tunafunguka” amesema Kifunda.
Mkurugenzi huyo amesema mradi huo utatoa elimu kwa watoto wa kike mashuleni kwa kuomba muda maalumu wa kuwafundisha wasichana wanaotarajia na ambao tayari wamepevuka, kwa wazazi ili waweze kuzungumza na watoto wao pamoja na kusambaza pedi za bei nafuu kupitia wajasiriamali watakaofundishwa ili kila msichana aweze kumudu kuzipata.
Akieleza madhara ya kutozungumzia suala la hedhi, Bw. Kifunda amesema kuwa, wasichana wamekuwa wakipata shida wanapokuwa katika siku za hedhi na kwa sababu hakuna mawasiliano katika hilo wanajikuta wakitumia karatasi, majani ya miti, pamba n.k katika kujisitiri hivyo kusababisha magonjwa ya kansa na ugumba.
Amesema kwa kipindi cha miezi mitatu ya majaribio ya awali ya mradi lengo ni kufikia shule 6, watoto wa kike 700, wazazi 600 na wajasiriamali wanawake wanne watakaosambaza pedi za bei nafuu katika Wilaya za Kishapu na Shinyanga.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Bw. George Andrea kwa niaba ya Serikali ya Mkoa, ameishukuru “Thubutu Africa Initiative” kwa kubuni mradi huo ambao amesema utawanufaisha watoto wengi wa kike na kuwa Serikali itakuwa bega kwa bega na wadau hao katika kufanikisha adhma ya kusaidia watoto wa kike Mkoani Shinyanga.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bw. Mohamed Kahundi amekiri kuwa ni kweli utoro mashuleni bado ni changamoto na tatizo kubwa kwa watoto wa kike ni hedhi.
Hivyo amewasisitiza wadau hao kutimiza lengo la kusaidia watoto wa kike ili wasome katika mazingira bora na kuinua elimu yao bila kubadili nia na mipango ya Serikali.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa