Na. Paul Kasembo, KAHAMA.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa mtoto akimjua Mwenyezi Mungu itasaidia sana kupunguza mmomonyoko wa maadili kwani watakuwa wameishi na kutenda yale yote yanayoelekezwa na dini zetu ambayo kimsingi ndiyo mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwetu sote na ndiyo maadili ya Kitanzania huku akipongeza kwa mkutano mkubwa wenye hadhi ya Kimataifa.
RC Macha ameyasema haya leo katika hitimisho la Mkutano wa Waadventisti Wasabato Ukanda wa Dhahabu wenye hadhi ya Kimataifa uliofanyika Kanisa la Sabato Nyahanga Wilayani Kahama mkutano uliopewa jina la "KAHAMA NET EVENT 2024, YATOSHA JANGWANI" na kushuhudiwa na maelfu ya watu ndani na nje ya nchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kutafsiriwa kwa lugha ya Kinyarwanda, Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu.
"Pamoja na pongezi nyingi kwa kuandaa mkutano huu wenye hadhi ya Kimataifa, lakini kubwa zaidi niseme tu kwamba Watoto wetu wakilelewa katika misingi ya kumjua Mwenyezi Mungu hakika itapunguza sana mmomonyoko wa maadili katika jamii," amesema RC Macha.
Katika hotuba yake pia amepongeza kwa umahiri mkubwa uliotumika kuandaa mkutano huu mkubwa wenye hadhi ya Kimataifa ambao umerushwa kwa lugha yetu ya Kiswahili na hivyo kuitangaza lugha yetu na nchi Kimataifa kutokea Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga, huku akisisitiza kuwa jambo hili limeipatia heshima kubwa lugha na nchi yetu na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote likiwemo la Wasabato.
Kwa upande wa risala iliyosomwa kwa niaba ya uongozi wa Kanisa imesema kuwa mkutano huu ulioanza rasmi tarehe 11 Mei, 2024 umeweza kutoa mafundisho mbalimbali ikiwemo Malezi ya watoto na familia, ujasiliamali, afya na afya ya akili umehitimishwa leo tarehe 1 Juni, 2024 huku kanisa likitoa ombi maalum la kupatiwa eneo litakaloweza kujengwa Kituo cha Vivutio na nyumba za watumishi wa Kanisa hapa Kahama jambo ambalo RC Macha amelipokea na kuridhia.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa