Katibu msaidizi , ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Magharibi Ndg. Gerald A. Mwaitebele amewataka viongozi wa umma kanda ya magharibi kukamilisha ujazaji na kuwasilisha matamko ya rasilimali na mali zao kama sheria inavyowataka kabla ya Desemba 31, 2023.
Mwaitebele ameyasema hayo leo tarehe 10 Desemba, 2023 wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maadili ambapo kwa Kanda ya Magharibi imetekelezwa mkoani shinyanga kwa kutembelea na kugawa zawadi mbalimbali kwa watoto na akina mama wodi ya wazazi katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (MWAWAZA), kutoa mafunzo ya maadili kwa watendaji wa kata, mitaa na vijiji Manispaa ya shinyanga.
Aidha Mwaitebele akiwa ameongozana na watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa shinyanga (TAKUKURU) walifika Chuo cha Ushirika Moshi tawi la Shinyanga (KIZUMBI) ambapo walifanya kongamano ambalo lilikuwa na mada mbalimbali ikiwemo "Nini kifanyike ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili na vitendo vya rushwa nchini" ikiwa ni pamoja na kuimarisha misingi ya Maadili kwa wanachuo chuoni hapo kwa lengo la kuwapa uelewa zaidi.
Baada ya hapo Mwaitebele na wataalamu hao walipanda miti ya matunda chuoni hapo ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha maadhimisho haya kwa ushirikiano na uongozi wa chuo, wanafunzi pamoja na wadau wa maadili.
"Tunapohitimisha maadhimisho haya, niwakumbushe viongozi wa umma wote kanda ya magharibi kuzingatia misingi ya maadili ikiwa ni pamoja na kuwasilisha tamko la rasilimali, MASLAHI na madeni kabla ya tarehe 31 Desemba, 2023 kama sheria inavyowataka," Mwaitebele.
Kwa upande wake muwezeshaji kutoka TAKUKURU ndg. Mohamed Doo ameaema kuwa uwepo wa elimu ya maadili ya viongozi wa umma katika nyanja mbalimbali ikiwomo taasisi za elimu, afya, serikali na klabu za maadili kunatajwa kuwa na tija zaidi, kwani wakielimika wataipenda nchi yao, watatenda haki nk.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa