Na. Paul Kasembo, Ihelele Misungwi.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi Kahama Shinyanga KASHWASA kwa namna inavyotekeleza utunzaji wa Usafi na Mazingira katika chanzo chake cha maji kilichopo Ihelele Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza huku akitoa wito kwa wale wanaodaiwa ankara za maji kulipa kwa wakati ili kuiwezesha Mamlaka kutoa huduma iliyo bora na stahiki kwa wananchi.
RC Macha ametoa pongezi hizi leo tarehe 18 Mei, 2024 alipotembelea na kuona namna ambavyo Mamlaka inavyoendesha Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria na kuuza maji ya jumla kwa Mamlaka nyingine zinazohusika na usambazaji wa maji kwa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini. Aidha, wateja wa Mamlaka ya Maji KASHWASA wamegawanyika katika makundi matatu (3) ambayo ni Mamlaka za Maji Mijini (WSSA), Jumuiya za Watoa Huduma ya Maji (CBWSO) na Mgodi.
"Nawapongeza sana kwa namna ambavyo mnachapa kazi hii ya kutoa huduma muhimu kwa maisha ya watu, lakini kwa dhati kabisa nawapongeza zaidi kwa utunzaji mkubwa wa mazingira katika chanzo hiki cha maji Ihelele hongereni sana KASHWASA," amesema RC Macha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka Eng. Patrick Nzambaamesema kuwa KASHWASA inazalisha maji kiasi cha lita 80 Milioni kwa siku ambapo baadhi ya miundombinu inaweza kupanuliwa na kuongeza uwezo wa kuzalisha maji hadi kufikia lita 120 milioni kwa siku na kutoshereza mahitaji ya watu zaidi ya 1,900,000 pamoja na mifugo yao kwa Mikoa sita (6) ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida na Geita huku ikitajwa kutoa huduma kwa saa 23.5 kwa siku.
Aidha, Mamlaka ya Maji KASHWASA iliiundwa kwa Tangazo la Serikali Na. 45 la mwaka 2007 na inatimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira Na.5 ya mwaka 2019 pamoja na maeneo mengine yaliyoongezwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 359 la mwaka 2023.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa