Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Rais UTUMISHI kwa kushirikiana na Mradi wa uimarishaji wa mifumo ya Sekta ya Umma nchini PS3 wamezindua mfumo wa dawati la malalamiko katika ngazi ya Mkoa kwa lengo la kutekeleza dhana ya utawala bora.
Uzinduzi huo umefanyika mwishoni mwa wiki hii katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa bw. Burton Mwakanyamale, Maafisa Utumishi na Utawala Ofisi ya Rais TAMISEMI na UTUMISHI, Meneja Mradi wa PS3 Mkoa, Bi. Joyce Mfinanga, Mratibu wa PS3 Sekretarieti ya Mkoa, Wakuu wa Sehemu na Vitengo pamoja na baadhi ya watendaji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mfumo huo utawawezesha wananchi kulalamika kwa njia rahisi zaidi, kwani kutakuwa na Ofisi maalumu ya Malalamiko itakayokuwa na Afisa mahsusi wa kupokea malalamiko yote, fomu maalumu za malalamiko zitakazopatikana katika tovuti ya Mkoa na tovuti za Halmashauri ambayo wananchi wataipakuwa na kujaza kisha kuiwasilisha ofisini, Aidha, kutakuwa na simu ambayo wananchi watapiga kuwasilisha malalamiko yao.
Mshauri wa masuala ya Utawala bora wa Mradi wa PS3 Dkt. Nazar Sola amesema katika Sera utawala bora, kuwawezesha wananchi kutoa malalamiko ni mojawapo ya uimarishaji wa Sera hiyo muhimu kwani inasaidia kutatua matatizo na kero za wananchi katika ngazi za awali na mapema zaidi.
Dkt. Nazar amesema mfumo huu wa malalamiko ambao utamilikiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI, umeanzishwa katika mikoa minne ya Kigoma, Dodoma, Mtwara na Shinyanga. Amesema, kwa Mkoa wa Shinyanga mfumo unafanyiwa majaribio katika wilaya ya Kishapu na tayari umeshazinduliwa kwa kuanzisha ofisi au madawati ya malalamiko katika ngazi ya Halmashauri, Kata, vijiji, vituo vya afya, zahanati, Hospitali, shule ya msingi na Sekondari.
Naye Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi. Neema Nguku amesema mfumo wa dawati la malalamiko umekuja kutokana na mapungufu yaliyoonekana katika utaratibu wa maboksi ya maoni uliokuwepo ambapo ilibainika kuwa hayakutumika kikamilifu. Bi Neema amesema,baada ya mapungufu hayo Katibu Mkuu TAMISEMI alitoa maelekezo ya watumishi kuvaa beji wawapo kazini ili wananchi wapate nafasi ya kulalamika dhidi ya watumishi wasio waadilifu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa