Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Shinyanga wametakiwa kufuatilia sababu za kutotumika kwa fedha zinazotumwa na Serikali katika vituo vya kutolea huduma za Afya kwa lengo la kuboresha huduma.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela ametoa agizo hilo leo tarehe 04 Juni, 2018 wakati akifungua mafunzo ya maboresho ya mfuko wa Afya ya jamii (CHF), mfumo jazia pamoja na mfumo wa upelekaji wa fedha moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma za Afya ujulikanao kama “Direct Health Facility Fund (DHFF)”.
Msovela amewataka viongozi hao kusimamia matumizi ya fedha hizo, kufuatia kuwepo kwa changamoto kwa baadhi ya Halmashauri kutotumia fedha zinazotumwa na Serikali, kutumia nje ya utaratibu au kutoingiza matumizi katika mfumo wa kielekroniki wa usimamizi wa fedha kwenye vituo vya Afya.
“Ukiangalia kwa muda mrefu fedha hizi hazitumiki vizuri, shida ni usimamizi na watumishi kufanya kazi kwa mazoea na baadhi yao kufanya nje ya utaratibu na fedha nyingine hazitumiki au kutumika nje ya mfumo” amesema Msovela.
Amesema, kutotumika kwa fedha hizo maana yake ni kuwa wananchi hawapati huduma zinazostahili ikiwemo huduma ya dawa, hivyo kuwakosea haki.
Mafunzo hayo yanayoendeshwa kwa siku mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yana lengo la kuwasaidia wataalamu wa Afya kuwa na uelewa wa ugatuaji wa mipango na bajeti na kusimamia matumizi ya fedha hizo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa