Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewapongeza Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kwa kuendelea na usambazaji umeme kwa wananchi hasa vijijini vya Mkoa wa Shiinyanga ambapo vijiji 442 kati ya 506 vimewekewa huduma ya umeme.
CP Hamduni amesena haya kwenye Kikao cha TANESCO Mkoa wa Shinyanga na Wadau Wakubwa wa Umeme mkoani kilichofanyika Oktoba 3, 2024 kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama sanjari na wadau huku ikitajwa takwimu kuwa mpaka sasa jumla ya wateja 98,716 tayari wameunganishiwa huduma ya umeme ambapo kati ya hao wateja wakubwa ni 110.
“Sote tunatambua TANESCO Mkoa wa Shinyanga imeendelea kuimarisha huduma za umeme vijijini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Jumla ya vijiji 442 kati ya 506 vimefikiwa na umeme. Ni matarajio ya Serikali kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024 vijiji vyote vilivyobaki (64) vitakuwa vimefikiwa na miundombinu ya umeme," amesema CP. Hamduni.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mha. Leo Mwakatobe pamoja na kuwashukuru lakini amewashauri wateja wao kurekebisha mifumo yao ya umeme kwenye maeneo yao ili waweze kulipa bili halisi kulingana na matumizi yao.
“Tunataka muimarishe mifumo yenu ya umeme ili kupunguza malalamiko ya ongezeko la bili za umeme, rekebisheni mifumo yenu ili mulipe pesa kulingana na huduma mnazopata, tunataka tuwatoze fedha kulingana na matumizi halisia”, amesema Mha. Mwakatobe.
TANESCO Mkoa wa Shinyanga limekutana na Wateja wakubwa wa umeme wakiwemo Wamiliki wa Viwanda na Migodi lengo likiwa ni kuwashukuru, kusikiliza, kupokea maoni kwa lengo la kuboresha huduma za umeme kwa wateja pamoja na kutoa Vyeti kwa wateja wakubwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa