Na. Paul Kasembo - USHETU.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ametembea katika Kata Igwamanoni iliyopo Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama ili kuwajulia hali waathirika wa mvua pamoja na kuhimiza ujenzi wa nyumba bora zenye kuanza na msingi wa mawe, tofali za kuchoma au za saruji ili kukabiliana na athari zitokanazo na mvua zinazoendelea.
Haya yametolewa leo tarehe 20 Aprili, 2024 ambapo RC Macha awali alitaarifiwa kuwa zaidi ya nyumba mia tano (500) zimeathirika na mvua huku kaya 21 zikiwa zimekosa kabisa makazi ya kuishi ambapo athari hizi imetajwa kutokea katika nyakati tofauti tofauti huku tarehe 10 Aprili, 2024 ndiyo kunatajwa kuwa nyumba nyingi zaidi ziliathirika zaidi na hivyo kufika idadi hii.
Pamoja na kuwashukuru sana ndugu na jamaa wote waliojitolea kuwahifadhi wahanga wa mvua hizi, RC Macha amesema kuwa, Serikali haitawaacha wapate shida na hivyo amemuagiza DC wa Wilaya ya Kahama kufanya tathimini ya amhao bado hawajapata usaidizi wa aina yoyote ili waone namna ya kuwasaidia.
"Tumekuja kuwapa pole nyote mlioathirika na mvua hizi zinazoendelea hivi sasa pamoja na kuwapa salamu za Serikali kuwa ipo nanyi wakati wote, lakini pia kuwataka nanyi muanze ujenzi wa nyumba bora zenye kuanza na msingi wa mawe chini, tofali walau za kuchoma na hasa ziwe za saruji ili kuweza kukabiliana na janga la aina yoyote ikiwemp maafa yatokanayo na mvua nyingi," amesema RC Macha.
Awali akitoa taarifa ya uwepo wa maafa yatokanayo na mvua hizi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita amesema kuwa, katika athari hizi Kata ya Igwamanoni iliyopo Ushetu ni moja kati ya maeneo ambayo wananchi wake wameathirika sana na mvua hizi, ambapo pamoja na kupoteza baadhi ya makazi lakini pia miundombinu ya barabara imeharibika zaidi hasa kati ya Igwamanoni na Kata ya Luhaga iliyopo mpakani mwa Mbogwe - Geita.
Kando na maelekezo haya, pia RC Macha ametoa siku 4 kwa TARURA Wilaya ya Kahama kuhakikisha kuwa wanarekebisha na kurejesha mawasiliano ya haraka kupitia baarabara ya Igwamanoni hadi Luhaga ambayo imeathirika zaidi jambo ambalo linapelekea kukatika kwa mawasiliano kabisa ili wananchi waendelee kupata huduma.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa