Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, amewashauri wananchi mkoani Shinyanga kujenga utamaduni wa kupima Afya zao mara kwa mara, huku akimpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini.
RC Macha amebainisha haya leo Juni 18, 2024 wakati alipotembelea kuona Maendeleo ya ujenzi wa uboreshaji wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, pamoja na utoaji huduma za Afya kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia ambao wanaendelea na utoaji wa matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa hapa mkoa wa Shinyanga.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakisumbuliwa na Magonjwa na kufikia katika hatua mbaya, hali ambayo inasababishwa na kutopima Afya mara kwa mara, ili kupata ushauri wa Daktari kwa kulinda Afya au kuanza Tiba mapema.
“Wananchi nimeona mmejitokeza kwa wingi kuja kupata Matibabu kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo natoa wito kwa wananchi wa Shinyanga mjenge tabia ya kuchunguza Afya zenu mkiwa bado wazima na siyo kusubili hadi mnakuwa katika hali mbaya,”amesema Macha.
“Mkipima Afya zenu mapema itawasaidia kujua hali zenu, na ukibainika unatatizo unaanaza matibabu mapema na kupona, Mfano Magonjwa haya ya Saratani ya Matiti na Shingo ya kizazi ukiwahi matibabu mapema unaweza kupona kabisa,”ameongeza Macha.
Aidha, amesema katika Shinyanga watapanga namna ya kuweka utaratibu wa wananchi wawe wanapima afya zao mara kwa mara, huku, akiwataka pia wananchi wakate Kadi za Bima za Afya ambazo zitawasaidia kupata matibabu kwa urahisi bila ya kuingia gharama kubwa na kuokoa Afya zao.
Katika hatua nyingine amempongeza Rais Samia kwa kutoa fedha na kuboresha huduma za Afya nchini, ikiwamo na Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, ambayo kwa sasa ujenzi wake unakwenda kukamilika kwa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), najengo ya upasuaji na Wodi.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk. Elisha Robert amesema ujenzi wa uboreshaji wa Hospitali hiyo ya Manispaa ya Shinyanga utakamilika Juni 30, 2024.
Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya, huku wakiwaletea pia Madaktari Bingwa na kuwapatia Matibabu ya Kibingwa na kuimarisha Afya zao.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa