Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha mapema leo tarehe 27 Novemba, amefika Kituo cha Kupiga Kura kilichopo Mtaa wa Lubaga Farm hapa Manispaa ya Shinyanga na kupiga kura kutimiza haki hake ya Kikatiba huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupiga kura na kurudi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali ambapo baadae watatangaziwa matoke.
RC Macha ametoa wito huu leo ikiwa ni siku maalum ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo wananchi wamepata nafasi ya kuchagua Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji, Vitongoji, pamoja na wajumbe, wao ambao watawatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano hadi 2029.
"Leo hii ndiyo siku pekee ambayo tumekuwa tukiisubiria sana ambapo kila mwananchi aliyejiandikisha, mwenye vigezo anapaswa kupiga kura kuwachagua viongozi wetu ambao watahudumu kwa miaka mitano kuanzia leo, hivyo niwakumbushe wananchi kutumia muda kwenda kupiga kura na kisha kuendelea na shughuli zetu za kila siku na matokeo watatangaziwa," amesema RC Macha.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Kanda ya Serengeti ndg. Jackson Mnyawami ambaye naye alifika hapa kupiga kura amesema kuwa zoezi la Uchaguzi katika kituo hiki lipo vizuri na linakwenda salama huku akiomba maboresho kwa baadhi ya vituo huku akitoa wito kwa wanachama na wananchi kujitokeza kutumia haki yao muhimu ya Kikatiba ili kuwapata viongozi wao.
Katika Kituo hiki cha Lubaga Farm, pamoja na wananchi mbalimbali kufika hapa Kupiga Kura lakini pia amefika Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Serengeti ndg. Jackson Mnyawami ambao wote kwa nyakati tofauti wametimiza takwa la Kikatiba la kuchagua viongozi wao.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Mkoa wa Shinyanga unajumuisha Mitaa 130, Vijiji 506, Vitongoji 2704 na utakuwa na Vituo vya Kupiga Kura 3080.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa