Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Agosti 18,2025 ametembelea eneo la tukio katika Mgodi wa Nyandolwa uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, na kukutana na ndugu wa wachimbaji waliokwama chini ya kifusi baada ya mgodi huo kutitia, ajali iliyohusisha mafundi takribani 25.
Katika mkutano huo, RC Mhita alitoa pole kwa familia na ndugu wa waathirika, akisisitiza kuwa serikali ya mkoa iko pamoja nao wakati huu mgumu na inaendelea kuchukua hatua zote za haraka kuhakikisha shughuli za uokoaji zinafanikiwa.
"Tunahitaji kila sekunde kuokoa maisha, juhudi zinaendelea usiku na mchana na tunawaombea wote waliopo chini ya kifusi wawe hai,” alisema RC Mhita.
Mhe. Mhita alibainisha kuwa Serikali tayari imeanza kutoa msaada wa chakula kwa wanafamilia walioko kwenye Mgodi huo wanaogojea kuokolewa kwa ndugu zao 18 ambao bado wamekwama chini ya kifusi ili kuwapa faraja wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.
Kwa mujibu wa RC Mhita, hadi sasa watu 7 wameokolewa kutoka kwenye kifusi, ambapo kwa masikitiko makubwa, 4 kati yao wamethibitika kupoteza maisha, na wengine 3 wakiwa hai na wanaendelea kupatiwa huduma za matibabu. Hii inafanya idadi ya mafundi waliobaki chini ya kifusi kufikia 18.
Mafundi hao walikuwa wakitekeleza kazi ya ukarabati wa mgodi unaomilikiwa na kikundi cha Mchapakazi, kwa ajili ya kuanza tena uzalishaji, kabla ya ajali hiyo kutokea na mgodi kutitia ghafla.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa