Sabasaba 2025.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, @mboni_mhita ametoa pongezi kwa Mamlaka ya Uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa juhudi na mafanikio wanayoendelea kuyapata katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hususan kwenye maeneo maalum ya kiuchumi.
Akizungumza alipofanya ziara kwenye banda la TISEZA katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayofanyika katika Viwanja vya J.K Nyerere, Barabara ya Kilwa – Dar es Salaam, Mhe. Mhita alisema kuwa TISEZA ni mfano wa Taasisi zinazotekeleza kikamilifu dhamira ya Serikali ya kuimarisha uchumi wa viwanda kupitia uwekezaji wa kimkakati.
"Napenda kuwapongeza TISEZA kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mmekuwa sehemu muhimu ya kuhakikisha Tanzania inanufaika kikamilifu na fursa za kiuchumi zinazotokana na maeneo maalum ya uwekezaji," alisema Mhe. Mboni.
Katika mazungumzo yake na Maafisa wa TISEZA, RC Mboni alitumia fursa hiyo kuwakumbusha kuhusu uwepo wa maeneo kadhaa maalum ya uwekezaji mkoani Shinyanga. Alieleza kuwa Mkoa umejipanga vilivyo katika kutangaza fursa hizo kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza ushirikiano wa karibu na TISEZA katika kuzivutia rasilimali na mitaji ya maendeleo.
“Mkoa wa Shinyanga una ardhi kubwa, miundombinu inayoimarika, na nguvu kazi ya kutosha. Huu ni wakati wa kuhakikisha maeneo yetu maalum yanajulikana na kuvutia wawekezaji wa kweli,” aliongeza RC. Mboni.
Mazungumzo kati ya RC Mboni na uongozi wa TISEZA yamejikita zaidi katika njia bora za kuhamasisha uwekezaji na kukuza maendeleo ya kiuchumi mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya kukuza viwanda, ajira, na kuongeza pato la taifa kupitia Sekta binafsi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa