Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa juhudi thabiti katika kusimamia na kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na maadili miongoni mwa watumishi wa Mahakama nchini.
Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama wa Mkoa wa Shinyanga na wilaya zake, Mhe. Mhita alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanawajengea uwezo wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi, haki na uadilifu.
“Mafunzo haya yana umuhimu mkubwa kwa sababu yanatoa fursa ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati za Maadili kutekeleza majukumu yao kwa haki na uadilifu. Tunatambua kuwa maadili bora ndiyo nguzo ya haki na msingi wa imani ya wananchi kwa chombo cha Mahakama,” alisema Mhita.
Aliongeza kuwa bila maadili thabiti, heshima na hadhi ya Mahakama hubakia mashakani, hivyo akasisitiza kuwa juhudi za Tume hiyo zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa haki.
Aidha, RC Mhita alieleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga itaendelea kushirikiana kwa karibu na Mahakama katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa usawa na bila upendeleo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama anayeshughulikia Maadili, Bi. Alesia Mbuya, alisema kuwa tangu ziara ya Jaji Mkuu Mstaafu Prof. Juma Ibrahim kufanyika mkoani Shinyanga mwezi Novemba 2022, Tume imeendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati za Maadili ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Alibainisha kuwa ziara hiyo ililenga kukutana na watumishi wa Mahakama, Kamati za Maadili pamoja na wadau wa mnyororo wa haki, kwa lengo la kubadilishana mawazo na uzoefu kama njia mojawapo ya kudumisha ushirikiano.
Bi. Mbuya aliongeza kuwa Tume imekuwa ikiendesha mafunzo na uratibu wa karibu kwa Wajumbe wa Kamati hizo ili kuhakikisha maadili ndani ya Mahakama yanadumishwa kwa kiwango cha juu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa