Na Johnson James, Kahama
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewafariji wafanyabiashara waliopoteza mali zao kufuatia janga la moto lililotokea usiku wa kuamkia octoba 26, katika Mtaa wa Igalilimi, Kata ya Kahama Mjini, na kuahidi kuwa Serikali ya Mkoa itashirikiana nao katika kipindi hiki kigumu kwao.
Akiwa ameambatana na viongozi wa kamati ya Usalama na baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Manispaa Kahama, Mhe. Mhita leo Octoba 26. 2025 alitembelea eneo la tukio ambapo moto huo uliteketeza maduka sita kati ya 13 yaliyoko katika jengo hilo.
“Nawapa pole sana kwa hasara hii kubwa. Najua mmeathirika kiuchumi na kisaikolojia, lakini niwahakikishie kuwa Serikali ipo pamoja nanyi,” alisema Mhe. Mhita.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara wote mkoani Shinyanga umuhimu wa kujikinga na majanga ya moto kwa kufunga vitambuzi vya moto (smoke detectors) na kuwa na vifaa vya kuzimia moto katika kila jengo la biashara.
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, ASF Fatma Sato, alisema moto huo ulisababishwa na hitilafu ya umeme katika moja ya maduka, na ulienea kwa haraka kutokana na bidhaa zinazowaka kwa urahisi kama magodoro, vitambaa na nguo.
Amesema kikosi chake, kwa kushirikiana na wananchi pamoja na kikosi cha zimamoto cha Mgodi wa Barrick Buzwagi, walifanikiwa kudhibiti moto huo , jambo lililosaidia kuokoa maduka saba yasiteketee.
Mmiliki wa jengo, Bi. Febronia Ikombe, alishukuru ujio wa Mkuu wa Mkoa na akaahidi kutekeleza agizo la kufunga vifaa vya tahadhari ya moto.
Mmoja wa wafanyabiashara, Bw. Paul Hamka, alisema ujio wa Mkuu wa Mkoa umewapa faraja kubwa na motisha ya kuanza upya.
Moto huo haukusababisha vifo wala majeruhi, lakini ulibainisha umuhimu wa tahadhari katika maeneo ya biashara.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa