Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, leo Agosti 18, 2025 amewapokea rasmi madaktari bingwa tisa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) waliofika mkoani hapa kwa ajili ya kutoa huduma maalum za afya kwa wananchi.
Zoezi la kuwapokea madaktari hao limefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, likihudhuriwa na viongozi wa sekta ya afya mkoani hapa pamoja na wawakilishi wa wataalamu wa JKCI.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Mhita amesema ujio wa madaktari hao ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya mkoani hapa na kusaidia wananchi kupata matibabu ya kibingwa bila kulazimika kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam.
"Tunawakaribisha kwa moyo wa shukrani madaktari wetu bingwa. Huduma hizi ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wetu, hasa wenye matatizo ya moyo na kina mama wanaohitaji uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi," amesema Mhita.
Huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo itakayofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni pamoja na uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zoezi ambalo linaenda sambamba na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kwa kina mama. ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha afya za wananchi kwa kuwafuata walipo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wamesisitiza kuwa kambi hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuimarisha ustawi wa jamii kupitia huduma jumuishi.
Kambi hiyo inatarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa muda wa siku tano ikianza Agosti 18 hadi 22, 2025, ambapo wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufaidika na huduma hizo muhimu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa