Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na maombi kwa ajili ya Taifa.
Mhe. Mhita ameyasema hayo katika Maulid ya Mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika Septemba 14,2025 katika Uwanja wa Shycom, Manispaa ya Shinyanga, ambapo alihimiza waumini na wananchi kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi katika kipindi hiki nyeti cha uchaguzi Mkuu.
“Tuendelee kuiombea nchi yetu ipite salama kipindi hiki. Uchaguzi ni zoezi muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu, tusikose kushiriki. Lakini pia tuendelee kuishi kwa kutegemea ibada, tukidumisha Amani na mshikamano bila kujali tofauti zetu za kiitikadi,” alisema Mhita.
Katika Maulid hayo, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga aliwaongoza waumini kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuomba nchi iendelee kuwa na amani, umoja na ustawi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, wa kisiasa, watendaji wa serikali na mamia ya waumini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na kudhihirisha mshikamano wa kitaifa kupitia imani.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa