Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amekabidhi misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, nguo na vifaa vya ujenzi vilivyotolewa na wananchi wa Shinyanga kwa waathirika wa mafuriko ya tope yaliyoambatana na mawe kutoka Mlima Hanang' katika wilaya ya Hanang' Mkoani Manyara na kuwaomba kuendelea kumshukuru, kumuomba na kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kila jambo.
RC Mndeme ameyasema haya leo tarehe 22 Des, 2023 wakati wa kukabidhi misaada kiwa kwa Mkuu wa wilaya ya Hanang Mhe. Janeth Mayanja ambapo pamoja na pole kwa wana Hanang' lakini pia alitoa pole kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tukio hili lililoathiri mali na kupelekea vifo.
"Msaada tunaotoa ni mdogo ukilinganisha na madhara yaliyotokea, hivyo tunaomba hiki kilichotolewa na wanashinyanga mkipokee," RC Mndeme.
"Shinyanga ni sehemu ya watanzania, tuliposikia janga hili tulipokea kwa masikitiko makubwa sana, kwa mapenzi mema waliyonayo wanashinyanga wakaona nao wamuunge mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na pia wawaunge mkono wananchi wenzao kwa kutoa pole kwa wanaHanang hivyo tumefika hapa katika mji huu wa Katesh kuwasilisha kwako mhe. DC pole zetu ili kuonesha umoja na kwamba tuko pamoja katika kipindi hiki kigumu ambapo kwa wenzetu wa Hanang wanapitia," amesema Mhe. Mndeme.
Kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga ambao wamejitolea kutoa pole zao kwa ndugu zao wa Hanang, RC Mndeme amekakibidhi mifuko 1000 ya saruji, mchele kilo 700, unga wa mahindi kilo 355, unga lishe kilo 250, juisi za matunda mbalimbali katoni 500, chumvi pakti 90, sukari kilo 25, sabuni katoni 13, mafuta ya kupikia lita 5, viatu jozi 43, Belo za nguo 30 kati ya hizi 27 ni nguo za wanaume na belo 3 nguo mchanganyiko.
Kwa upande wake DC Wilaya ya Hanang Mhe. Janeth Mayanja amemshukuru RC Mndeme kwa niaba ya wanashinyanga wote kwa ,huruma, utu, upendo, ubinadamu na undugu wa kweli waliouonesha kwa wanaHanang na kwamba msaada huu ni sehemu ya kumuunga mkono kwa vitendo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kadhia hii iliyowakumba wanahanang'.
HABARI PICHA
RC Mndeme wa pili kutoka kulia, akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi wa kwanza kulia, akifuatiwa na DC wa Katesh aliyesimama kushoto akifuatiwa na DC Mboni Mhita wa Kahama
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa