Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Solomon Mndeme ameitaka kampuni Sinohydro Company Limited iliyopewa kandarasi ya kujenga Mradi wa Umeme wa Jua wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 323 unaotekelezwa katika kijiji cha Ngunga Wilaya ya Kishapu hapa mkoani Shinyanga kukamilisha ujenzi huu kwa wakati, kwa kuzingatia ubora, viwango, muda waliokubaliana na bila kuongeza bajeti ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya uhakika ya umeme.
Mhe. Mndeme amemuagiza Mkandarasi huyu leo tarehe 29 Oktoba, 2023 alipokuwa akizungumza na wadau wa mradi huu, baadhi ya wananchi waliopisha mradi huu kijijini Ngunga, viongozi mbalimbali, pamoja na watumishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Tanesco huku akimsisitiza kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wa ngunga, kishapu na shinyanga kwa ujumla katika mradi huu muhimu.
"Nikuombe (Sinohydro Co. Ltd) mkandarasi uliyepewa dhamana ya kujenga mradi huu mkubwa wa umeme hapa kijiji cha ngunga Kishapu, ukamilishe mradi huu kwa wakati na kwa kuzingatia muda, viwango, thamani na bajeti tuliyokubaliana ili wananchi waanze kunufaika na uwepo wa mradi huu," alisema Mhe. Mndeme.
Awali akiwakaribisha wadau wa mradi huu ambao ni Shirika la Maendeleo la Ufaransa AFD group - Dar es salaam Agency Mndeme aliwaeleza kuwa serikali itafanya kazi nao bega kwa bega, itawapatia ushirikiano wakati wote na pia aliwashukura sana kwa ujio wao kuja kuona eneo litakalotekelezwa mradi huu mkubwa wa umeme.
Mhe. Mndeme kipekee kabisa alimshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mradi huu mkubwa wa umeme ha hasa kuja kutekelezwa katika kijiji cha ngunga kilichopo Wilaya ya Kishapu hapa mkoani Shinyanga, mradi wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 323 fedha za kitanzania.
Kwa upande wake Eng. Emmanuel Anderson kutoka Tanesco na ambaye ndiye mhandisi na msimamizi wa mradi huo kwa (MW 50) Ngunga - Kishapu alisema kuwa mradi huu utatekelezwa ndani ya miezi 14 na kwamba mkandarasi yupo tayari na sasa iliyobakia ni kuanza kazi tu.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa