Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina S. Mndeme leo tarehe 19 Novemba, 2023 ameongoza wananchi, viongozi wa dini, serikali na chama katika kutoa heshima ya mwisho kwa Salu Ndongo aliyekuwa Afisa Ardhi Mfawidhi Manispaa ya Shinyanga tukio lililofanhika katika Kanisa la Waadventista Wasabato lililopo Shinyanga huku akiwakumbusha kuishi kwa utayari kwani hatujui siku wala saa ambapo tutakumbwa na umauti.
Mhe. Mndeme amesema kuwa, alipokea kwa mstuko taarifa ya msiba huu kwakuwa alikuwa akimfahamu na uchapa kazi wake na kwamba serikali inatoa pole sana kwa wanajumuiya ya shinyanga manispaa kwa ujumla kwa msiba huu, na kumsihi Mjane wa marehemu na kumtaka kushikilia zaidi msalaba pamoja na kumtumainia Yesu kwakuwa yeye ni mfariji wakati wote na baba wa Yatima na Wajane.
"Ndugu zangu, msiba huu unatukumbusha kuishi kwa utayari kwani hatujui siku wala saa umauti nasi utatukuta, pia tuendelee kumtumainia Mungu wakati wote," alisema Mhe. Mndeme.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato Razalo Mbogo amesema kuwa, yeye binafsi amemfahamu kwa muda mrefu sana marehemu Ndongo, na kwamba alikuwa mchapakazi anayehudumia wananchi kwa haraka na kwa uzalendo zaidi na ndiyo maana msiba huu umegusa wananchi wengi zaidi.
Marehemu Salu Ndongo alifariki tarehe 17 Novemba, 2023 kwa ajali ya gari aliyokuwa akiendesha mwenyewe katika eneo la kalogo manispaa ya shinyanga na mazishi yatafanyika kijijini kwao Gangabilili, wilaya ya Itilima - Simiyu.
......Raha ya milele umpe eebwana, apumzike kwa amani Salu Ndongo...Amin
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa