Na. Shinyanga RC.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amesema kwamba Mwenge wa Uhuru ambao utakimbizwa mkoani humo utazindua, kukagua pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo 42 yenye thamani ya Bilioni 13.4.
Mwenge wa uhuru katika Mkoa wa Shinyanga unatarajiwa kupokelewa Julai 27 mwaka huu, na utakimbizwa katika Halmashauri sita za mkoa huo, ambazo ni Kishapu, wilaya ya Shinyanga, ushetu, Msalala, Manispaa ya Kahama na Shinyanga.
Mndeme alibainisha hayo juzi wakati akikagua miradi ya maendeleo ambayo itapitiwa na Mwenge huo wa Uhuru katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Kahama.
Alisema, ameridhishwa na Maandalizi ya Miradi ya Maendeleo ambayo itatembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri hizo mbili za Shinyanga na Kahama, na kwamba ziara hiyo ni endelevu kwa kutembelea halmashauri zote kuona miradi ambayo itapitiwa na Mwenge wa Uhuru.
"Nimetembelea miradi ya Elimu,Afya,Mazingira, Kilimo, Miundombinu, na uwezeshaji wananchi kiuchumi miradi yote ni mizuri," alisema Mndeme.
Aidha, aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wajitokeze kwa wingi kuupokea Mwenge huo wa Uhuru, ambapo utakuwa ukipita katika maeneo yao pamoja na kuwazindulia Miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Manispaa ya Kahama Sadick Kigaile, alitaja Miradi ya Maendeleo ambayo itapitiwa na Mwenge wa Uhuru ni Miradi ya Kilimo, Shamba la Miti, Ofisi ya Kata Nyihongo, Jengo la Maabara Hospitali ya wilaya Kahama, miundombinu ya Barabara, na uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake kiuchumi na shule ya Sekondari kagongwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Miradi ambayo itapitiwa na Mwenge wa Uhuru ni Kikundi cha Vijana Wabunifu Kata ya Busanda, Mashine ya kukomboa nafaka na kuongeza thamani ya Mazao Kata ya Didia, na kikundi cha Ufugaji nyuki pamoja na Miradi ya Elimu na Afya.
Picha ikimuonesha Mhe. Christina Mndeme kushoto akiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Ndg. Anderson Msumba wakikagua jengo la uchunguzi wa magonjwa na mionzi
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa