Na. Shinyanga RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amewapongeza sana Asasi ya Kusaidia Sekta Binafsi za Kilimo yaani Private Agricultural Sector Support - PASS kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Sekta ya Kilimo huku akiwataka kuongeza kasi ili kuweza kuwafikia wakulima wote hasa vijana kundi ambalo ni kubwa ambalo likiwezeshwa zaidi litaleta tija kubwa kwa kuinua na kuboresha kipato kwao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo tarehe 08 Agosti, 2023 alipokuwa akihutubia wakulima, wananchi, viongozi wa Serikali, Dini na wadau mbalimbali katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Ziwa Mashariki katika viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu ambapo Mhe. Mndeme ndiye alikuwa Mgeni Rasmi huku akisisitiza kuwa ili Taifa letu liweze kupiga hatua kiuchumi lazima tuanze kwa kuwabadilisha watu wetu ki-fikra hasa vijana na wanawake wafanye kazi kwa bidii na maarifa ili kukuza uchumi wao na kuchangia maendeleo ya taifa letu.
"Nawapongeza sana PASS TRUST kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Sekta ya Kilimo kwa Kanda ya Ziwa Mashariki lakini niwatake sasa kwenda kuongeza kasi katika kuwafikia wakulima wote hasa vijana, kundi hili mkilifikia kwa ukubwa wake mtakuwa mmesaidia sana kuwainua kiuchumi na kuongeza ajira kwa vijana nchini," alisema Mhe. Mndeme.
Kando na pongezi hizo, pia Mhe. Mndeme amewataka Taasisi ya Kudhihiti Ubora wa Mbegu Tanzania - TOSCI kufuatilia na kufanya utafiti wa kutosha katika eneo la mbegu bora zinazohimili changamoto ziweze kutumika kwa wakulima wetu.
Pia aliwaelekeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania - TARI kufanya tafiti ya kina ili kujuwa na kubaini zaidi magonjwa yanayoathiri mazao na kuyatafutia ufumbuzi wake kwa haraka, na pia aliwataka Bodi ya Pamba kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wakulima katika maeneo yao, kwakuwa kumekuwepo na tatizo la uchafu kwa baadhi ya zao la pamba.
Mhe. Mndeme pia amewahimiza sana wananchi kulima, kupanda na kutumia zaidi mchicha aina ya URUSI, mboga ambayo inatajwa kuwa na virutubisho vingi na bora zaidi kwa afya ya wananchi wetu huku akiwapongeza sana PASS TRUST kwa kuwa mshindi wa jumla katika maadhimisho haya lakini pia pongezi kwao kwa kuwa wadhamini wakuu wa sherehe za nanenane kwa Kanda ya Ziwa Mashariki 2023.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Nanenane ya mwaka huu wa 2023 yamebeba Kauli Mbiu isemayo "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula".
RC Mndeme akiwa amepanda moja kati ya Trekta zilizopo kwenye Banda PASS TRUST katika maonesho ya nanenane viwanja vya Nyakabindi Bariadi Mkoani Simiyu
RC mndeme akiwa katika banda la Pass Trust
RC mndeme katika moja kati ya Banda la mifugo linalomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)
Picha na matukio
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa