Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mboni Mhita kupitia kwa mwakilishi wake Wakili Julius Mtatiro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, amezitaka halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kuwa zinayasimamia ipasavyo Mabaraza ya Wazee na kuyawezesha kwa kutenga bajeti mahsusi, kuwashirikisha katika vikao vya maamuzi, pamoja na kuhakikisha wazee wanapata huduma bora za afya.
Mtatiro ametoa maelekezo hayo Septemba 23, 2025, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Jomu, Kata ya Tinde, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
“Nawaagiza Wakurugenzi wote wa halmashauri kuhakikisha wanatenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za wazee na kuwashirikisha wawakilishi wa mabaraza yao kwenye vikao vya maamuzi. Ni muhimu wazee wetu wakahusishwa katika ujenzi wa jamii,” amesema Mtatiro.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Shinyanga una jumla ya wazee 100,626. Kati ya hao, 43,256 wamepatiwa kadi za matibabu bila malipo, sawa na asilimia 43, na wengine 11,063 wamepatiwa kadi za CHF, sawa na asilimia 11.
“Nazipongeza halmashauri zilizofanikiwa kutoa kadi za matibabu kwa wazee bila malipo. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha wazee wanapata huduma bora za afya,” ameongeza Mtatiro.
Aidha, ameagiza halmashauri zote kuhakikisha kila robo mwaka zinafanya ukaguzi wa dawa na fedha kwenye vituo vya kutolea huduma, kuagiza dawa kwa wakati, na kuhakikisha dawa kwa makundi ya msamaha zinakuwepo ili kuondoa usumbufu kwa wazee.
Akihitimisha hotuba yake, Mtatiro ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, 2025, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Ni haki ya msingi ya kikatiba kushiriki uchaguzi. Tuende tukapige kura kwa amani na tuilinde nchi yetu dhidi ya vurugu,” amesisitiza.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu: “Wazee Tushiriki Uchaguzi Mkuu kwa Ustawi wa Jamii Yetu.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa