Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amezindua kampeni ya Kitaifa ya kuhamasisha wananchi kujenga vyoo bora na kuvitumia leo tarehe 03/09/2019, katika uwanja wa Zimamoto, eneo la Nguzonane, Manispaa ya Shinyanga inayojulikana kwa jina la usichukulie poa, Nyumba ni choo.
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Mhe. Telack amewataka Maafisa Afya wa Halmashauri zote Mkoani hapa kuwasilisha mpango kazi wa kuhakikisha kila nyumba ina choo kufikia Desemba mwaka huu.
Aidha, Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia Maafisa Tarafa na Watendaji wa kata na vijiji vyote wahakikishe wanapata taarifa za kaya ambazo hazina vyoo na hatua gani zimechukuliwa.
“Kufikia mwezi Desemba mwaka huu, tuwe hatuzungumzii mtu kutokuwa na choo tena, Mkoa una asilimia 50.6 tu ya vyoo bora. kwa hiyo turudi tujipange vizuri kuwa na vyoo bora” amesema Telack.
Mhe. Telack ameishukuru Wizara ya Afya na wadau Benki ya Dunia kwa kufanikisha Kampeni hii iliyoanza mwaka 2012 na kusema kuwa, ni kazi kubwa imefanyika kufikia asilimia zaidi ya 50 ya wananchi wanaotumia vyoo kutoka asilimia 17.
Awali, akitoa taarifa ya hali ya vyoo katika Mkoa, Afisa Afya wa Mkoa Bi. Neema Simba amesema, mila potofu ikiwemo ya marufuku wakwe kuchangia choo kimoja inachangia wananchi kujisaidia vichakani.
Naye Balozi wa Kampeni hiyo Bw. Mrisho Mpoto amesema, haiwezekani Mkoa kuacha shughuli nyingine za uzalishaji na kuzungumzia kujenga vyoo, hivvo kila mwananchi akawe balozi kwa mwingine kuhusu kuwa na vyoo bora na kuvitumia.
Aidha, Mrisho amewahamasisha wananchi kuachana na kasumba potofu ya kuonesha uwezo wa chakula kwenye kaya kwa vinyesi kusambaa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amesema ni jambo linawezekana kabisa kwa Mkoa wote kila kaya kuwa na choo bora, iwapo viongozi katika kila ngazi watajipanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa