Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Kamishna Msaidizi wa Polisi Debora Magiligimba ametoa angalizo kwa watendaji wanaoshiriki kuwaficha watuhumiwa wanaowapatia mimba watoto wa shule na wanaofanya ukatili kwa watoto kuwa wataingia kwenye matatizo.
Akizungumza katika kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack na Watendaji wa kata, Maafisa Elimu kata pamoja na Wakuu wa shule za msingi na sekondari leo tarehe 04/02/2020 kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Mwalimu Nyerere, Magiligimba amesema kuwa, kuna baadhi ya watumishi wanashiriki kuwafumbia macho watuhumiwa hao.
"Natoa angalizo kwa Watumishi wanaojiingiza kwenye hili, mtaingia kwenye matatizo. Kwa kipindi hiki cha mapambano ya mimba za utotoni, tupeni taarifa, tutawakamata wote" amesema.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa kuhakikisha wazazi wote wanaowazuia watoto kwenda sekondari wanakamatwa mara moja.
"Kamata wazazi wote ambao watoto wao hawajaripoti shule hadi sasa na dhamana ya kutoka ni watoto wao kwenda shule" amesisitiza Mhe. Telack.
Aidha, katika kikao hicho Telack ametoa rai kwa walimu wa kike kufanya kazi kwa kujiamini bila kuyumbishwa na mtu yeyote kwa sababu za kimapenzi.
"Hakuna mtu atakufukuza kazi kwa sababu ya kumkatalia kimapenzi. Ukiona kiongozi anakujia vibaya njoo kwangu, nitawalinda kwa nguvu zote, simameni imara" amesema Telack.
Amesisitiza pia kuwa na mahusiano mazuri ya kikazi ili kuepukana na migogoro isiyo ya lazima.
Mhe. Telack amemaliza ziara yake katika Halmashauri ya Msalala leo, ambapo kesho ataendelea kwenye Halmashauri ya Mji Kahama.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa