Dar es salaam.
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imefanya mageuzi makubwa kwa kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma kwa watoto wachanga.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo leo Jumamosi, Septemba 7, 2024 wakati akizungumza na viongozi na wadau walioshiriki mbio za hisani za 2024 zilizoandaliwa na Benki ya Maendeleo (Maendeleo Bank Marathon 2024) katika viwanja vya Green Park, Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
"Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati na afua mahsusi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa watoto wachanga. Ni jambo la fahari sana kuwa hivi sasa huduma maalum za watoto wachanga na ile ya Mama Kangaroo hadi kufikia Julai 2024, zimeanzishwa katika hospitali 245,” amesema Mhe. Majaliwa.
Waziri Mkuu amesema mafanikio haya yametokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inapunguza vifo vya watoto wachanga kufikia lengo namba tatu la Maendeleo Endelevu la vifo chini ya 12 katika kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2030 kutoka vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000 kwa mwaka 2022.
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya tukio hilo ambayo ni Hatua ya Faraja - Msimu wa Pili, Waziri Mkuu amesema kaulimbiu yao inasawiri mpango wa Benki hiyo wa kuendeleza kazi yao ya mwaka jana ya ununuzi wa vitanda maalumu vya kutunzia watoto njiti (Infant Baby Warmer) katika Hospitali ya KCMC.
Sambamba na ujenzi wa kituo kipya cha watoto wenye changamoto ya ulemavu wa akili na usonji kinachotarajiwa kujengwa wilayani Bagamoyo
“Kama mlivyosikia, pale KCMC, idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa njiti ni kubwa na ipo kati ya asilimia 20 mpaka 25. Hawa ni binadamu wenzetu wanaostahili kuishi na tuna kila sababu ya kuonesha upendo kwa kuchangia hatua za faraja.
"Hivyo basi, nitoe wito kwa wananchi wote wenye mapenzi mema kuendelea kuiunga mkono Benki ya Maendeleo katika utekelezaji wa afua hizi muhimu,” amesisitiza.
Amewapongeza viongozi wa benki hiyo kwa kuongeza lengo la uchangiaji kwenye mbio za mwaka huu kutoka sh. milioni 120 hadi sh. milioni 200 ili kukamilisha kazi waliyoianza mwaka 2023.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa