Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangala amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia na kuhakikisha kila kijiji kinatenga maeneo yatakayohifadhiwa kwa ajili ya kuhifadhi misitu na kuunda kanuni na taratibu za kiasili za kulinda maeneo hayo.
Mhe. Kigwangala ametoa agizo hilo jana, akizungumza na wanachi katika kuhitimisha kilele cha maadhimisho ya Upandaji Miti kitaifa yaliyofanyika katika uwanja wa Mji mdogo Mhunze, Wilaya ya Kishapu.
Sambamba na hilo ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuchagua Mikoa 10 itakayotakiwa kuanza utekelezaji wa agizo hilo ikiwemo Mikoa ya Shinyanga, Tabora na mingine inayokabiliwa na athari za uharibifu wa misitu ya asili.
Amewataka kutoa elimu kwa Serikali za vijiji waelewe umuhimu wa kuhifadhi maeneo na kuyalinda wakati Wizara ikiwa katika mchakato wa kuandaa na kuleta mwongozo kuhusu utunzaji wa maeneo hayo.
Mhe. Kigwangala amesema kuna mabadiliko makubwa yametokea tangu mwaka 2010 hadi sasa, kutokana na kukata miti, kuharibu misitu ya hifadhi, kuvamiwa vyanzo maji, kuanzishwa vijiji vipya,
“Uharibifu wa mazingira unakuwa kwa kiwango kikubwa, tusipokuwa macho taifa litaangamia tutakosa mvua, maji ya kunywa, malisho na chakula. Tutaishi wapi” amesema Kigwangala na kuongeza kuwa, idadi ya watu inaongezeka kila mwaka lakini ardhi ni ileile hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya hasa hasa kupanda miti.
Kigwangala amesema kuwa, hivi sasa ukataji wa miti kwa mwaka kwa mahitaji mbalimbali ni kati ya ekari 800 elfu hadi milioni 1. 2. Kwa hali hiyo inatakiwa kupanda miti milioni 300 mfululizo kila mwaka kwa mika 17 ili kufikia nusu ya kiwango cha uharibifu unaofanywa kwa mwaka mmoja tu.
Maadhimisho ya upandaji miti Kitaifa yamefikia kilele chake jana Wilayani Kishapu ambapo Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni “ Tanzania ya Kijani inawezekana, tupande miti kwa maendeleo ya viwanda”
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa